Na mwandishi wetu
Wapinzani wa Simba SC, Raja Casablanca wametua nchini mchana wa leo tayari kwa mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo ya Morocco imetua kwenye Uwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) huku wachezaji wake wakionekana na furaha na zaidi wakisisitiza wanaifahamu Simba wakijua ni timu kubwa lakini wamekuja kupambana kutafuta pointi.
Raja wametua wakiwa wanaongoza Kundi C kwa pointi tatu baada ya kuibuka na ushindi wa nyumbani wa mabao 5-0 dhidi ya Vipers ya Uganda, ikitegemea upinzani mkali kutoka kwa Simba.
Simba katika mechi hiyo itaingia uwanjani kwa nia ya kupambana ili kuvuna pointi tatu za kwanza baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Horoya ya Guinea kwenye mechi ya kwanza.
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesisiiza kuwa jeshi lake liko tayari kuwakabili Raja na kuchukua pointi tatu katika mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi hii.
Robertinho amesema kinachompa matumaini ya ushindi katika mchezo huo ni utimamu na utayari waliokuwa nao wachezaji wake ambao wameonesha nia ya wazi kutaka kushinda mchezo huo.
“Dhamira yetu ni moja tu kwenye mchezo huo, pointi tatu bila kujali ukubwa na ubora wa mpinzani sababu hata Simba ni timu bora ndio maana imefika hatua hii na watu wajue kwenye hatua tuliyopo hakuna timu ndogo,” alisema Robertinho raia wa Brazil.
Kocha huyo amesema kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kama Saido Ntibazonkiza, Jonas Mkude na Peter Banda kumemuongezea nafasi pana ya kuchagua kikosi kitakachoanza na kumpa matokeo mazuri kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi nchini.
Simba itaingia uwanjani ikiwa nafasi ya tatu katika kundi lake ikiwa haina pointi sawa na Vipers inayoburuza mkia huku Horoya ikiwa nafasi ya pili na pointi tatu kama Raja lakini ikizidiwa kwa mabao ya kufunga.