London, England
Arsenal jana Jumatano usiku ililala kwa mabao 3-1 mbele ya Man City na kushushwa kileleni, lakini kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta amesema imani kwa timu yake kubeba taji imeongezeka.
Timu hizo kwa sasa zote zina pointi 51, City ikiwa na faida ya mabao ya kufunga na kufungwa ingawa Arsenal ina pungufu ya mechi moja ikiwa imecheza mechi 22 dhidi ya 23 za City.
Arsenal, kwa muda mrefu imekuwa ikishika usukani wa ligi, inaonekana kuyumba baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi ya tatu mfululizo lakini Arteta amesema imani kwa wachezaji wake inazidi kuwa kubwa licha ya kushushwa kileleni.
“Wana imani, naliona hilo, wanaamini wanaweza kupata mafanikio,” alisema Arteta ambaye katika mechi iliyopita timu yake iliyoka sare ya bao 1-1 na Brentford matokeo yaliyozua utata.
Katika mechi ya jana, City walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Kevin De Bruyne kwa pasi ‘tamu’ ya Takehiro Tomiyasu lakini Bukayo Saka akasawazisha kabla Jack Grealish na Erling Haaland hawajafunga mabao mawili yaliyoihakikishia City pointi tatu.
“Nimeendelea kuwa na imani zaidi kuliko kabla ya mechi, kwa kiwango cha uchezaji kilichooneshwa na aina ya timu tuliyocheza nayo, tulijipa imani kwamba tungewafunga, hadi wanapata bao la pili tulikuwa vizuri,” alisema Arteta.
“Lakini mwisho wa siku tuliwapa mabao matatu, kuna makosa ambayo hutakiwi kuyafanya lakini hapo hapo timu ilijitoa katika kiwango cha juu, walipata nafasi tatu wakazitumia, tulipata nafasi nyingi hatukuzitumia vizuri,” alisema Arteta.
Arteta alikiri kwamba wamekatishwa tamaa kwa kufungwa lakini walicheza na timu bora duniani na kulingana nao katika kiwango cha uchezaji.
“Nina imani zaidi ya kubeba taji la ligi kwa sababu nimeona timu ilivyokabiliana nao, ni lazima twende kwenye mechi nyingine na katika siku tatu zijazo tuna mechi nyingine, nina imani zaidi na wachezaji wangu,” alisisitiza Arteta.