Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Melis Medo amewaomba radhi wadau wa soka na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), kwa kitendo chake cha kumpokonya mwamuzi wa kati kadi na kumpa mwamuzi wa akiba.
Tukio hilo lilitokea kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro ambapo katika dakika ya 38 mwamuzi wa mchezo huo alikwenda kumuonesha kadi ya njano Medo baada ya kutoa maneno machafu.
Baada ya kuoneshwa kadi hiyo, Medo (pchani juu) akionekana kujawa hasira alimpokonya mwamuzi huyo kadi hiyo na kumuonesha mwamuzi wa akiba.
Baada ya kitendo hicho mwamuzi wa kati alichukua uamuzi wa kumpa kadi nyekundu na kocha huyo raia wa Marekani kuondoka kwenye benchi la timu hiyo ambayo hatimaye ilifungwa mabao 2-1.
Kocha huyo amekiri kuwa tukio alilolifanya halikuwa la kiungwana na anaomba radhi kwa wale wote ambao hawakupendezwa na kitendo hicho.
“Ilikuwa ni hasira katika kuipigania timu yangu lakini ukweli najutia na pia naomba radhi kwa waamuzi wa mchezo husika, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi na wadau wote wa soka nchini kwa kile kilichotokea, binafsi nakijutia,” alisema Medo.
Kocha huyo ameeleza kuwa tukio hilo halitojirudia tena sababu yeye ni muumini mzuri wa kufuata kanuni na sheria zinazouongoza mchezo wa soka.
Medo amejiunga na Dodoma Jiji hivi karibuni akichukua mikoba ya Masoud Djuma aliyefutwa kazi kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC.