Na mwandishi wetu
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, imelisogeza mbele ombi la wanasheria wa mchezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ la kutaka kupitia upya shauri la mteja wao kuvunja mkataba na klabu ya Yanga.
Awali, pande hizo mbili zilikuwa zikutane Februari 16, makao makuu ya TFF, Karume jijini Dar es Salaam lakini shauri hilo limeelezwa kusogezwa mbele hadi Februari 28, mwaka huu.
Wakili anayemwakilisha Fei Toto, Salum Nduruma amekiri kupokea taarifa ya TFF ikiwaarifu kusogezwa mbele shauri hilo sababu kubwa ikitajwa kuwa tarehe husika wajumbe wa kamati watakuwa na majukumu mengine.
“Tumepokea taarifa ya kusogezwa mbele kwa pingamizi letu na tumeridhia kutokana na sababu ambazo tumepewa na TFF, kwa hiyo tutaendelea kusubiri hadi siku husika ambayo naamini ukweli utajulikana,” alisema Nduruma.
Nduruma alisema wameamua kufanya hivyo ili kuokoa kipaji cha mteja wao ambacho kwa sasa kimemuathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na kutocheza mechi za ushindani, jambo linalofifisha kiwango chake cha soka.
Januari 7, mwaka huu kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilisikiliza shauri hilo lililowasilishwa na Yanga wakipinga Fei kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu na baada ya kulipitia walibaini mapungufu.
Baada ya kubaini mapungufu kamati hiyo iliamua kumrudisha mchezaji huyo Yanga, kitendo ambacho jopo la wanasheria wa mchezaji huyo pamoja na mchezaji mwenyewe hawakukubaliana nayo.