Na mwandishi wetu
Timu ya Ihefu FC imemtambulisha kocha mkongwe, John Simkoko kuwa kocha wake mkuu baada ya kumsainisha mkataba wa miezi sita kuanzia leo Februari 12, 2023.
Simkoko anatua Ihefu akichukua mikoba iliyoachwa na Juma Mwambusi aliyeachana na timu hiyo tangu mwanzoni mwa mwezi Januari, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Athuman Mndolwa ameeleza kuwa wamevutiwa na kocha huyo kutokana na uzoefu wake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Tumefikia makubaliano na mkongwe Simkoko katika kipindi cha miezi sita ambapo kuna makubaliano ya kuurefusha mkataba, ni kocha mzuri kutokana na uzoefu wake. Imani yetu ni kwamba atatusaidia kufikia malengo ambayo tumejipangia,” alisema Mndolwa.
Mndolwa alisema kuwa Simkoko atasaidiana na Zuber Katwila katika kukinoa kikosi chao ambacho kwa sasa kinashika nafasi ya nane kwenye msimmao wa Ligi Kuu NBc wakiwa wamekusanya pointi 29 katika michezo 23.
Kabla kutua Ihefu, Simkoko amewahi kuipa ubingwa wa Ligi Kuu timu ya Mtibwa Sugar mwaka 2000 lakini pia miaka ya hivi karibuni amewahi kuzifundisha timu za Polisi Tanzania na KMC.