Na mwandishi wetu
Baada ya kuwasili mjini Tunis, Tunisia jana Yanga ilianza mazoezi ya kuondoa uchovu ili kuweka mwili imara na tayari kwa mchezo wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ya nchini humo utakaochezwa Jumapili hii.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema anajua mchezo ulioko mbele yao namna utakavyokuwa mgumu na ndio maana waliona wafanye mazoezi ya kuondoa uchovu kuweka mwili sawa.
Alisema kwa mazoezi waliyoanza nayo jana na leo anaamini watafanya vizuri katika mchezo huo wa kwanza kabla ya kurejea nchini kuvaana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mchezo wa pili utakaochezwa wiki ijayo.
“Tunajua kuwa tuna mchezo mgumu mbele yetu, tuna imani kwamba kama tutajiandaa vizuri, tutakuwa kwenye njia sahihi ya kuelekea katika mchezo wetu dhidi ya US Monastir.
“Tumeanza na mazoezi ya kuondoa uchovu mwilini kwa sababu tumetoka safari ya masaa 12, masaa sita kutoka Dar es Salaam hadi Dubai na masaa sita kutoka Dubai hadi Tunisia, inabidi tufanye mazoezi haya kuuandaa mwili, kujenga mwili,” alisema Kaze.
Kaze alisema aina ya mazoezi hayo husaidia sio tu kuimarisha mwili bali huwaweka wachezaji pamoja kabla ya mechi.
Yanga ilifuzu hatua ya makundi baada ya kuindosha Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa mwisho wa mtoano ngazi za awali kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0, ushindi walioupata ugenini.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema hali ya hewa ya Tunisia ni nyuzi joto tisa hivyo, baridi ni kali sana kama sio mwenyeji wa eneo hilo.
Kamwe alisema hiyo ndio sababu kubwa ya viongozi wa Yanga kuhakikisha timu inafika mapema huko ili wachezaji wapate kuzoea hali ya hewa kabla ya mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Olimpiki Hammadi mjini Tunis.