Madrid, Hispania
Mabosi Ligi Kuu Hispania au La Liga wanaazisha uchunguzi kwa mashabiki ambao wameendelea kumzomea na kumdhihaki kwa maneno ya ubaguzi wa rangi mchezaji wa Real Madrid, Vinicius Junior.
Vinicius kwa mara nyingine amekumbana na dhihaka hizo Jumapili iliyopita katika mechi dhidi ya Real Mallorca, mechi ambayo Real Madrid ilijikuta ikilala kwa bao 1-0.
Picha za video zilizopatikana kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha mashabiki wanaoaminika kuwa wa Mallorca wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Son Moix, wakitoa maneno ya dhihaka dhidi ya Vinicius.
Vinicius mwenye umri wa miaka 22 hapo kabla amejikuta katika dhihaka hizo za kibaguzi mara tatu tofauti kuanzia Nou Camp katika mechi dhidi ya Barcelona iliyopigwa Novemba, 2021.
Baada ya hapo, Vinicius alidhihakiwa kwa mara nyingine Septemba 2022 katika mechi dhidi ya Atletico Madrid na kukumbana tena na kadhia hiyo Desemba 2022 katika mechi dhidi ya Valladolid.
“Kutokana na tukio lililotokea katika mechi ya RCD Mallorca na Real Madrid, mechi ambayo kwa mara nyingine zimesikika kauli za udhalilishaji wa ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa Real Madrid, Vinicius Jr., La Liga inaweka nyenzo zote ilizonazo kuhakikisha wahusika wanabainishwa ili kuchukua hatua stahiki,” ilieleza taarifa ya La Liga.
Mallorca haikutoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo ingawa akihojiwa na chombo kimoja cha habari, kocha wa timu hiyo, Javier Aguirre alishutumu kauli za ubaguzi wa rangi zilizotolewa dhidi ya Vinicius.
Kocha huyo hata hivyo alikanusha habari kwamba wachezaji wake walilenga kumchezea rafu Vinicius ambaye alichezewa rafu mara 10, idadi ambayo ni kubwa kwa mchezaji yeyote wa La Liga kuivumilia.