London, England
Klabu ya soka ya Manchester City imeingia matatani baada ya uchunguzi kubaini kuwa imekuwa ikienda kinyume na kanuni za matumizi ya fedha na huenda ikashushwa daraja au kunyang’anywa pointi.
Uchunguzi huo umebaini kuwa klabu hiyo imekuwa ikienda kinyume na matumizi ya fedha kwa miaka tisa kuanzia mwaka 2009, mwaka mmoja tu baada ya kampuni ya Abu Dhabi United Group kuwa mmiliki mwenye hisa nyingi.
Taarifa ya bodi ya Ligi Kuu England iliyopatikana Jumatatu hii jioni ilieleza kuwa tume huru iliyopewa jukumu hilo imehitimisha uchunguzi wake wa miaka minne na kubaini uvunjifu wa kanuni za matumizi ya fedha katika klabu hiyo.
Tume hiyo itafanya kikao chake bila kuingiliwa na kutoa adhabu ambayo huenda ikahusisha faini, kunyang’anywa pointi au hata kushushwa daraja.
Taarifa ya bodi hiyo ilieleza, “Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, bodi imethibitisha kuwasilisha katika tume tuhuma za uvunjifu wa kanuni za matumizi ya fedha uliofanywa na klabu ya Manchester City.”
Klabu hiyo inadaiwa kuvunja kanuni zaidi ya 100 zikiwamo zinazoitaka klabu kuwasilisha taarifa zake za kifedha ambazo zinatoa mwelekeo sahihi na kweli kuhusu uwezo wa kifedha wa klabu hiyo.
Sambamba na tuhuma hizo, Man City pia inalalamikiwa kwa kutotoa ushirikiano wakati wote wa uchunguzi wa tuhuma hizo.

Taarifa ya Man City kujibu tuhuma hizo ilieleza kushangazwa na tuhuma za uvunjifu wa kanuni za Ligi Kuu na kuitaka tume kuzingatia ushahidi uliopo dhidi ya tuhuma hizo wakati wakisubiri tuhuma hizo kufutwa moja kwa moja.
Man City iliwahi kulalamikia uchunguzi huo ikidai ulitokana na uvunjifu wa sheria za mitandao na udukuaji wa nyaraka na machapisho ya klabu, hiyo ni baada ya jarida moja la Ujerumani kutoa taarifa za kashfa hiyo mwaka 2018.
Julai 2020, Man City iliikatia rufaa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) adhabu ya kusimamishwa kushiriki mashindano kwa miaka miwili iliyotolewa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa).
Uefa waliipa Man City adhabu hiyo baada ya uchunguzi kubaini kuwa klabu hiyo ilikuwa ikivunja kanuni za matumizi ya fedha za shirikisho hilo kati ya mwaka 2012 hadi 2016.
Hoja kuu ya CAS kufuta adhabu hiyo ni kuwa ushahidi uliotolewa ulipita kipindi kinachotambulika kwa mujibu wa kanuni cha miaka mitano, kanuni ambayo kwenye Ligi Kuu England haipo.
Inadaiwa kwamba sakata hilo ndilo lililowashawishi mabosi wa Ligi Kuu England kuanzisha uchunguzi dhidi ya klabu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye ligi.
Tangu mwaka 2008, klabu hiyo iliponunuliwa na matajiri wa Abu Dhabi hadi sasa imeshashinda mataji sita ya Ligi Kuu England na imekuwa na makocha watatu tofauti, Roberto Mancini, Manuel Pellegrini na sasa Pep Guardiola.
Klabu ya Juventus ya Italia nayo imekumbwa na sakata linalohusisha uvunjifu wa kanuni za matumizi ya fedha hali iliyosababisha baadhi ya wakurugenzi kung’atuka na timu hiyo kunyang’anywa pointi 15 katika Ligi Kuu Italia yaani Serie A.
Kwa sasa Man City inashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England ikiwa imezidiwa na vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi tano. Kocha wa timu hiyo Guardiola aliwahi kunukuliwa akisema kwamba mabosi wake waliwahi kumhakikishia kwamba hawajafanya kosa lolote kauli ambayo inaweza kuwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo wanaohisi timu yao inaweza kunyang’anywa pointi.