London, England
Kipa na nahodha wa Tottenham Hotspur, Hugo Lloris atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki sita hadi nane kutokana na maumivu ya goti yanayomkabili.
Lloris ambaye pia alikuwa nahodha timu ya Taifa ya Ufaransa kabla ya kustaafu mwezi uliopita, aliumia Jumapili iliyopita katika mechi ya EPL dhidi ya Man City, mechi ambayo Spurs ilishinda kwa bao 1-0.
Baada ya kuumia kwa kipa huyo ambaye ana miaka 36, Spurs sasa itakuwa ikimtumia kipa wa zamani wa Southampton na timu ya Taifa ya England, Fraser Forster ingawa pia inaweza kuwatumia Brandon Austin na Alfie Whiteman lakini hawana uzoefu wa kutosha.
Spurs ambayo inashika nafasi ya tano kwenye EPL, Jumamosi itajitupa uwanjani kuumana na Leicester City katika mechi ya ligi hiyo na Jumanne itaumana na AC Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na hapana shaka Forster atakuwa golini katika mechi hizo.
Forster alisajiliwa Spurs majira ya kiangazi msimu uliopita akiwa mchezaji huru, hadi sasa ameidakia timu hiyo mechi moja tu ya EPL Desemba mwaka jana dhidi ya Brentford, mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Spurs kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu England ikiwa katika kupigania kucheza Ligi ya Maabingwa Ulaya msimu ujao.
Kimataifa Hugo Lloris nje wiki nane
Hugo Lloris nje wiki nane
Read also