Doha, Qatar
Aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Iran, Carlos Queiroz ametangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya Qatar akichukua nafasi ya Felix Sanchez.
Queiroz ambaye pia amewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Ureno, atainoa timu hiyo kwa mkataba unaofikia ukomo mwaka 2026 wakati wa fainali za Kombe la Dunia za nchini Marekani, Canada na Mexico.
Kocha huyo ambaye ana miaka 69, mbali na timu ya Iran ambayo alikuwa nayo kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 Qatar, pia amewahi kuzinoa timu za Taifa za Afrika Kusini, Colombia na Misri.
Queiroz pia amewahi kuwa kocha wa klabu za Real Madrid na Man United akiwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson pamoja na klabu kadhaa kabla ya kugeukia kuzinoa timu za Taifa.
Kwa sasa Queiroz anaingia katika kibarua cha kuinoa timu ambayo imeshiriki mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia 2022 ikiwa mwenyeji na hivyo atakuwa na kazi ya kuisaidia ifuzu fainali zijazo za 2026.
Kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022, Qatar ilipangwa kundi moja na timu za Senegal, Ecuador na Uholanzi lakini ilipoteza mechi zake zote za hatua ya makundi na kuaga fainali hizo mapema.
Mkataba wa Queiroz ulisainiwa mjini Doha jana jioni kati ya kocha huyo na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Qatar (QFA), Mansour Al-Ansari kwa niaba ya QFA.
Kimataifa Queiroz kocha mpya Qatar
Queiroz kocha mpya Qatar
Related posts
Read also