Na mwandishi wetu
Timu ya Simba itakwea pipa mapema kuifuata Horoya AC ya Guinea baada ya kumaliza mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa keshokutwa Jumapili dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Simba ambayo leo Ijumaa jioni inatarajia kuumana na Singida Big Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC, Jumapili hii itavaana na Hilal kwenye Uwanja wa Mpaka, Dar es Salaam.
Baada ya mechi na Hilal timu hiyo itaanza mchakato wa safari yake hiyo huku ikitarajiwa kuanza kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi Februari 11, mwaka huu kwa kuumana na Horoya.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema baada ya hivi karibuni kuchaguliwa kuendelea na nafasi hiyo, mipango wanayoendelea nayo ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano wanayoshiriki ikiwemo ligi hiyo ndiyo maana wanahitaji kutua mjini Conakry mapema kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo.
“Yapo ambayo tulishayaanza tangu awali na ilikuwa ni mipango endelevu ambayo iliandaliwa na klabu kwa hiyo tutaendelea kuzikita hapo jitihada zetu kwa maana sasa tupo kwenye mashindano ya ligi, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi yetu ya kwanza ni Februari 11.
“Kwa hiyo timu itaondoka kuelekea Conakry baada ya mechi ya Jumapili na Hilal, yaani baada ya kumalizika mchezo huo tutatoa ratiba ya timu kusafiri kwenda kwenye mechi yetu hiyo,” alisema Mangungu.
Simba ikimalizana na Horoya kwenye mechi itakayopigwa Uwanja wa Jenerali Conte, itaikabili Raja Casablanca ya Morocco Februari 18 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kuelekea Entebbe, Uganda kuumana na Vipers.