Madrid, Hispania
Kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois (pichani) amesema mchezaji mwenzake katika timu hiyo, Vinicius Junior anahitaji kulindwa zaidi baada ya kuchezewa rafu mbaya na Gabriel Paulista wa Valencia.
Vinicius alichezewa rafu hiyo jana Alhamisi usiku dakika ya 72 katika mechi baina ya timu hizo, mechi ambayo Real Madrid ilitoka na ushindi wa mabao 2-0 wafungaji wakiwa ni Marco Aensio na Vinicius.
Ushindi huo umefanya Real Madrid ipunguze tofauti ya pointi dhidi ya vinara Barcelona hadi kufikia tano kutoka nane huku Valencia ikilazimika kucheza na wachezaji 10 uwanjani baada ya Paulista kupewa kadi nyekundu hapo hapo.
“Ni lazima tumlinde Vini (Vinicius) ni mpambanaji uwanjani, anawasumbua wachezaji na mabeki hawalipendi jambo hilo,” alisema Courtois mara tu baada ya mechi hiyo.
“Ni katika mbinu zake na aina yake ya uchezaji, tunamhitaji kuifungua safu ya ulinzi, nafikiri amekuwa akikwatuliwa sana na leo (jana) nimefurahi kwa sababu mwamuzi alikuwa na busara kiasi cha kutosha hadi kumtoa Gabriel nje, mpira haukuwa eneo hilo, kadi nyekundu ilikuwa lazima.” alisema Courtois.
Kwa Vinicius (pichani chini) bao alilofunga katika mechi ya jana linakuwa la 50 katika mechi 200 za ushindani akiwa na jezi ya Real Madrid.

Naye kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alimzungumzia Vinicius akisema, “Katika utimamu wa mwili yuko vizuri, ni mchezaji anayepata tabu sana, katika kipindi cha pili amekimbia mara nyingi bila ya mpira, anaingia nyuma ya mabeki na hilo linaleta tofauti.”
“Jambo hilo linawaacha wachezaji wa timu pinzani wakiwa wamechoka baada ya mechi, Vinicius pia amekuwa mwenye kujaribu mara kwa mara, haachi kufanya hivyo,” alisema.
Akiizungumzia rafu aliyochezewa mchezaji huyo Ancelotti alisema kwamba ni tukio la kukatisha tamaa ambalo hata hivyo alisema ni mambo yanayotokea kwenye soka.
Real Maadrid kwa sasa inasubiri ripoti ya madaktari kuhusu wachezaji wake Eder Militao na Karim Benzema ambao walilazimika kutolewa kwa kuwa majeruhi.
“Militao tatizo lake kubwa kidogo kuliko Karim (Benzema), kesho (leo) tutaangalia ukubwa wa tatizo la Karim lakini Militao hatokuwa nasi Jumapili katika mechi na Real Mallorca, hiyo ni hakika,” alisema Ancelotti.