Na mwandishi wetu
Klabu ya Singida Big Stars imeeleza kuwa itamkosa kiungo wake mshambuliaji, Frederico Dario kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja akielezwa kuwa na majeraha.
Kiungo huyo amerejea kwao nchini Brazil takriban siku tano zilizopita huku akiwa hajatumika kwenye mechi kadhaa za timu hiyo za hivi karibuni.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza alisema hakuna mgogoro wowote unaoendelea baina yao kama inavyoelezwa kwenye duru mbalimbali isipokuwa ni masuala ya matibabu na amepewa ruhusa maalum.
“Dario amerudi kwao kutokana na majeraha ya mguu aliyonayo aliyoumia kwenye mechi za hivi karibuni na amekwenda huko akiwa na mwakilishi wetu ambaye ni mtaalam wa masuala ya afya.
“Tutamkosa Dario kwa muda kidogo, anaweza kukosekana kwa kipindi cha takriban mwezi mzima na itachukua muda kwa sababu pia atakuwa na mapumziko ya muda mfupi kisha atarejea kazini kama kawaida,” alisema Masanza.
Dario ameondoka wakati kikosi hicho kikiendelea na maandalizi ya kuivaa Simba kwenye mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu NBC, mechi inayotarajiwa kupigwa Februari 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.