Milan, Italia
Klabu ya soka ya Juventus imenyang’anywa pointi 15 baada ya uchunguzi kubaini kwamba ilikuwa ikikiuka taratibu za usajili siku za nyuma, Shirikisho la Soka Italia (FIGC) limethibitisha.
Juventus, klabu kongwe katika Ligi Kuu Italia au Serie A ilikuwa ikidanganya katika mahesabu yake na kunufaika kwenye usajili kinyemela na kwa adhabu hiyo sasa inashuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.
Katika kilichoonekana kuwa ni dalili mbaya, Novemba mwaka jana wajumbe wa bodi ya klabu hiyo akiwamo rais wa zamani, Andrea Agnelli na makamu rais, Pavel Nedved walijiuzulu katika nafasi zao.
Juventus imekana kufanya jambo lolote baya na imethibitisha azma yake ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Olimpiki ya Italia (CONI).
Adhabu ya kuinyang’anya timu hiyo pointi 15 ni kubwa kuliko ile ya pointi tisa ambayo ilipendekezwa na mamlaka zilizoendesha kesi hiyo.
Katika sakata hilo, mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Juventus. Fabio Paratici ambaye kwa sasa ni mkurugenzi mkuu wa soka wa Tottenham amefungiwa kwa miezi 30.
FIGC pia imempa Agnelli na ofisa mtendaji mkuu wa zamani wa Juventus, Maurizio Arrivabene adhabu ya kifungo cha miaka miwili wakati mkurugenzi wa sasa wa michezo wa klabu hiyo, Federico Cherubini amefungiwa kwa miezi 16.
Sambamba na hilo jumla ya watendaji 11 wa Juventus wamepewa adhabu akiwamo Nedved ambaye amefungiwa kwa miezi minane adhabu ambazo kwa mujibu wa FIGC zitahusisha pia Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) na Fifa na hivyo kuwa adhabu zinazohusika kote duniani.
Aprili mwaka jana klabu hiyo ilifutiwa mashitaka na klabu nyingine 10 ikiwamo Napoli ambayo inashika usukani katika Serie A pamoja na Paratici na Agnelli ambao walikuwa miongoni mwa maofisa 59 wa klabu waliofutiwa tuhuma mbalimbali lakini Desemba mwaka jana ofisi ya waendesha mashtaka mjini Turin iliamua kukata rufaa uamuzi huo baada ya ushahidi mpya kupatikana kutoka kwa wapelelezi wengine kuhusu matumizi ya fedha za klabu ya Juventus.
Juventus katika miaka 13 ya uongozi wa Agnelli, imebeba taji la Serie A mara tisa mfululizo lakini msimu uliopita klabu hiyo ilimaliza ligi katika nafasi ya nne na kupata hasara ya Pauni 220 milioni, ikiwa ni rekodi ya kipekee kwa klabu za soka Italia.
Mwezi uliopita, Uefa pia ilitangaza kuanza uchunguzi dhidi ya klabu ya Juventus inayodaiwa kwenda kinyume na taratibu za leseni za klabu pamoja na matumizi ya fedha yasiyo ya haki.
Kimataifa Juventus yaporwa pointi 15
Juventus yaporwa pointi 15
Read also