Na mwandishi wetu
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu leo Ijumaa amezindua rasmi kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Januari 29, mwaka huu.
Mangungu katika kampeni hizo jambo la kwanza ambalo ameanika ni ukweli kuhusu kuuzwa kwa basi la timu ya Simba jambo ambalo limekuwa likiibua maswali kila kukicha.
Mangungu amekiri kuwa basi la timu hiyo limeuzwa na sio bovu kama inavyoelezwa hoja ambazo zimekuwa mjadala ka muda mrefu kwa kuwa basi hilo halijaonekana huku wachezaji wakitumia basi dogo aina ya Coaster kabla ya kuthibitika leo kuwa limeuzwa.
“Nashushiwa lawama ambazo si zangu basi la Simba limeuzwa mimi nikiwa sipo kwenye uongozi sikuwa mjumbe wa bodi wala mwenyekiti wa timu hii kama nilivyo sasa,” alisema Mangungu.
“Lakini baada ya kuingia kwenye uongozi hili suala lilipelekwa kwenye bodi ya klabu na wajumbe tumelifuatilia na kubaini liliuzwa kwa kufuata utaratibu,” alisema Mangungu.
Kiongozi huyo anayemaliza muda wake katika nafasi hiyo amesema kama atapewa nafasi atahakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mashindano yote ikiwemo kufuta uteja kwa watani zao Yanga ambao siku za karibuni wamekuwa wakionewa na wapinzani wao hao.
Pamoja na hayo, Mangungu alisema ili kufanikisha hayo ni lazima kuwepo ushirikiano baina ya uongozi wa timu, wanachama na mashabiki ikiwa ni vitu vya msingi katika kukua kwa taasisi yoyote ile.
“Kipindi changu kinachomalizika wiki ijayo yapo mengi mazuri ambayo tulifanya kwa kushirikiana na mwekezaji pamoja na wanachama na hata mashabiki na tulifanikiwa, nakumbuka tulichukua ubingwa kwa timu ya wanaume na wanawake na kufika robo fainali Kombe la Shirikisho,”
“Msimu uliopita bahati mbaya tulipoteza ubingwa lakini ndio mchezo unavyokuwa ingawa kama tutaweka mbele umoja na mshikamano nafasi ya ubingwa bado tunayo msimu huu sababu nafasi tuliyopo kwenye msimamo na idadi ya mechi zinatupa nafasi hiyo,” alisema Mangungu.
Mangungu amesema mipango yake mingine ni kuiongezea hadhi klabu hiyo na kuwa klabu kubwa Afrika yenye mafanikio kama zilivyo Al Ahly, Zamalek na nyinginezo zinazofanya vizuri kwa sasa Afrika.
Mangungu ambaye anachuana na Moses Kaluwa katika nafasi hiyo ya uenyekiti ameeleza kuwa yapo mengi makubwa ambayo amekusudia kuyafanya pindi atakaporejea tena kwenye kiti hicho na hiyo ni kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa klabu hiyo.
Kiongozi huyo pia amemshukuru mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’ kwa kumpa ushirikiano na ujasiri aliokuwa nao wa kuwekeza pesa zake kwenye klabu hiyo na kuifanya kuwa tofauti na klabu nyingine nchini.
Pia aliwashukuru wajumbe wenzake pamoja na wapenzi na wanachama kwa ushirikiano katika kipindi chote alichokuwa madarakani ambapo kwa umoja wao walifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mambo mengi na amewaomba radhi pale ambapo aliwakosea.
Mangungu aliingia madarakani Febuari 7, 2021 katika uchaguzi mdogo uliofanyika kwa lengo la kuziba nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa wazi na Swedi Nkwabi aliyejiuzulu miezi 10 baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 5, 2018.