Cairo, Misri
Mabingwa watetezi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), Morocco huenda wakaadhibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kutotokea katika michuano ya CHAN inayoendelea nchini Algeria.
Kamati ya maandalizi ya michuano hiyo ilitangaza kwenye mkutano na waandishi wa habari Jumatatu kwamba watawasiliana na CAF ili kujua adhabu ambayo Shirikisho la Soka Moroco (FRMF) litapewa kwa kushindwa kupeleka timu kwenye michuano hiyo.
Mgogoro baina ya Algeria na Morocco unadaiwa kugusa masuala ya michezo na unatajwa kuwa chanzo cha timu ya Morocco kushindwa kushiriki michuano ya CHAN mwaka huu.
Algeria inadaiwa kutoruhusu anga lake kutumiwa na ndege iliyokuwa na timu ya Morocco kutua Algeria Januari 13 kwa ndege ya moja kwa moja.
Mabingwa watetezi Morocco waliotwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo Februari 2021, katika michuano ya mwaka huu walipangwa Kundi C na Madagascar, Sudan na Ghana na walisisitiza azma yao ya kusafiri na ndege ya moja kwa moja ya Royal Air Maroc kutoka jiji la Rabat na ujumbe wa nchi hiyo nchini Algeria ulifika uwanja wa ndege Ijumaa ili kuipokea timu hiyo.
Hata hivyo ruhusa ya kutua kwenye ardhi ya Algeria haikutolewa na mamlaka nchini Algeria zikishikilia msimamo wa kutoruhusu ndege ya moja kwa moja kutoka Morocco wakati huo huo Morocco nao wakishikilia msimamo wa kutokubali kuingia Algeria kupitia nchi nyingine.
Mazingira hayo ndiyo yanayoacha swali juu ya hatma ya timu hiyo CAF iwapo watapewa adhabu au Algeria wataingia lawamani kwa kuwazuia Morocco kuingia nchini humo kwa ndege ya moja kwa moja.
Sudan ambao walikuwa wacheze na Morocco Jumapili, waliingia uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo na kupewa pointi tatu na mabao matatu ya bure.
Mgogoro baina ya Algeria na Morocco unaweza kuziathiri nchi hizo ambazo pia kila moja inawania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) 2025 na ingawa Morocco ndiyo inayopewa nafasi kubwa lakini mgogoro unaoendelea unaweza kuikwaza nchi hiyo.
Kimataifa CAF kuiadhibu Morocco?
CAF kuiadhibu Morocco?
Read also