London, England
Bilionea wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe kupitia kampuni yake ya Ineos ameingia rasmi katika mbio za kuinunua klabu ya Manchester United baada ya familia ya Glazer kutangaza nia ya kuiuza klabu hiyo.
Awali bilionea Ratcliffe alitaka kuinunua Chelsea kwa Pauni bilioni 4.25, mpango ambao hata hivyo ulikwama na klabu hiyo kununuliwa na bilionea mwingine Todd Boehly.
Familia ya Glazer ilitangaza Novemba mwaka jana nia ya kuiuza klabu hiyo na kumuibua Ratcliffe ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuinunua klabu hiyo akibebwa na mambo kadhaa ikiwamo historia yake kwenye soka n tayari ameahidi kuwekeza kwa kila hali kuisaidia klabu hiyo.
Ratcliffe ambaye alipewa nafasi kubwa kuinunua Chelsea baada ya bilionea wa Urusi, Roman Abramovich aliyekuwa akiimiliki klabu hiyo kuiuza kutokana na vikwazo ambavyo nchi yake iliwekewa baada ya kuivamia Ukraine.
Baada ya mpango wa kuinunua Chelsea kukwama, Ratcliffe ambaye inadaiwa ni shabiki wa Man United tangu utotoni amepania kuhakikisha anainunua klabu hiyo huu ukiwa ni mkakati wa pili baada ya awali kukutana na ndugu wawili wa familia ya Glazer, Joel na Avram ambao walimkatalia.
Ratcliffe anayetajwa kuwa mmoja wa matajiri wa Uingereza, si mtu mgeni kwenye soka kwani kupitia kampuni yake ya Ineos wana hisa nyingi katika klabu za Nice ya Ufaransa na Lausanne ya Uswisi.
Familia ya Glazer ambayo imekuwa ikiimiliki Man United tangu mwaka 2005 katika miaka ya karibuni imejikuta ikitiwa misukosuko na mashabiki ambao hawaridhishwi kwa namna inavyosimamia klabu hiyo ikidaiwa kutojali ustawi wa klabu badala yake inachoangalia ni faida pekee.
Hali hiyo imekuwa ikiwakera mashabiki ambao wamekuwa wakielezea malalamiko yao dhidi ya familia hiyo ya nchini Marekani ikiwamo kufanya maandamano ya amani kupinga uendeshaji wa klabu hiyo.
Mei mwaka jana maelfu ya mashabiki wa Man United waliandamana hadi Old Trafford kuikataa familia ya Glazer hali iliyosababisha mechi ya Man United na Liverpool kuahirishwa kwa hofu ya kutokea vurugu.
Kampuni ya Raine inayosimamia mchakato wa kuuzwa kwa labu hiyo imeahidi hadi Februari kumaliza zoezi la kuchuja majina ya kampuni zinazowania kuinunua klabu hiyo na kubaki na chache kabla ya kukamilisha mchakato wa mauzo mwezi Machi.
Kimataifa Rasmi, Bilionea Ratcliffe kuinunua Man Utd
Rasmi, Bilionea Ratcliffe kuinunua Man Utd
Read also