Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix Minziro ameeleza amejiandaa vilivyo kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi ya keshokutwa dhidi ya Polisi Tanzania ili kuendelea kupigania ndoto za timu hiyo katika mechi zilizobaki za ligi.
Geita inatarajia kuwa mwenyeji katika mchezo huo unaotarajia kupigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Akizungumza na GreenSports, Minziro alisema anahitaji kuendelea kupata ushindi kama ilivyokuwa kwenye mechi yao ya mwisho walipoifunga Dodoma Jiji mabao 2-0 ingawa anaamini mechi ya Polisi itakuwa ngumu zaidi.
“Mechi ni ngumu na ligi ni ngumu pia lakini tunaendelea kujiweka sawa na tuko tayari kwa ajili ya Polisi, hakuna timu inayotaka kupoteza katika kipindi hiki ndiyo maana nasema ligi ni ngumu na tunafahamu hilo.
“Mara ya mwisho tulipata ushindi dhidi ya Dodoma, tunahitaji kuendelea na wimbi la ushindi japo sio kitu rahisi lakini kwa kuwa tunahitaji kupigania ndoto za Geita msimu huu inatupasa kuendelea kupambana kupata pointi tatu katika kila mechi,” alisema Minziro.
Geita inakutana na Polisi iliyo chini ya Mwinyi Zahera ikiwa nafasi ya tano na pointi 27 wakati Polisi ikiburuza mkia kwenye nafasi ya 16 na pointi zake 14.
Kocha wa Polisi, Mwinyi Zahera amenukuliwa hivi karibuni akijiaminisha kuwa timu hiyo haitoshuka daraja licha ya kuwa katika nafasi mbaya wakati ligi ikielekea ukingoni.