London, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kwamba hatoondoka katika klabu hiyo labda ikitokea akalazimishwa kufanya hivyo ingawa amegusia kuwapo kwa mabadiliko katika majira ya kiangazi.
Kauli ya Klopp, imekuja kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kiasi cha baadhi ya wachambuzi kuanza kutoa maoni kwamba siku za kocha huyo Mjerumani zinahesabika katika timu hiyo ya Anfield.
Liverpool kwa sasa inashika nafasi ya tisa kwenye Ligi Kuu England na iko nyuma kwa tofauti ya pointi 10 kati ya timu nne vinara hali ambayo inatia shaka iwapo itashiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
“Ni ama kutakuwa na mabadiliko kwenye nafasi ya kocha au mambo mengine mengi yatabadilika, lakini kwa upande wangu labda itokee mtu akaniambia niondoke, tofauti na hivyo siondoki,” alisema Klopp.
Klopp aliongeza, “hiyo maana yake ni kwamba labda inaweza kufika wakati tukataka kubadili baadhi ya watendaji, tutaona lakini hilo ni jambo la siku zijazo ni majira ya kiangazi au wakati wowote, si sasa hivi.”
“Nina muda wa kutosha na nafasi ya kulifanyia tafakuri jambo hilo, kwa sasa tunachotakiwa kufanya ni kucheza soka vizuri,” alisisitiza.
Jumamosi iliyopita Liverpool ilifungwa mabao 3-0 na Brighton, matokeo ambayo Klopp aliyaelezea kuwa ni kiwango kibaya cha uchezaji na kuongeza kuwa timu yake ni lazima irudi katika misingi yake ili kuboresha kiwango. Leo Jumanne timu hiyo itaumana na Wolves katika mechi ya Kombe la FA ambayo pia inatajwa kuwa kipimo kingine cha majaliwa ya Klopp katika timu hiyo.
Awali kocha huyo alinukuliwa akikana kuwa na upendeleo kwa baadhi ya wachezaji, “Ni kweli nimesikia hizo habari, nilisikia kabla na siko hivyo.”