Saudi Arabia
Kocha wa Barcelona, Xavi hatimaye amebeba taji lake la kwanza na timu hiyo baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid katika mechi ya fainali ya taji la Super Cup la Hispania.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Saudi Arabia jana Jumapi, kinda wa miaka 18 wa Barca, Gavi ndiye aliyeanza kwa kufungua kitabu cha mabao alipoandika bao la kwanza kwa pasi ya Robert Lewandowski kabla ya Lewandowski naye kuongeza bao la pili akiitumia pasi ya Gavi.
Gavi kwa mara nyingine ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao la tatu la Barca lililofungwa na Pedri kabla Karim Benzema hajaifungia Real Madrid bao pekee la kufutia machozi.
Gavi mbali na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kufunga bao katika mechi ya fainali ya Super Cup akiipiku rekodi ya kocha wake Xavi ambaye alikuwa mchezaji wa timu hiyo.
Kipa Thibaut Courtois ndiye aliyeiokoa Real Madrid kufungwa mabao mengi kwa jinsi alivyozuia michomo ya mara kwa mara langoni mwake hasa mapema kipindi cha kwanza alipojaribiwa na Lewandowski na Ousmane Dembele.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Oktoba mwaka jana katika El Clasico ya kwanza msimu huu, Real Madrid iliibugiza Barca mabao 3-1 lakini kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Barca imeendelea kuwa imara siku hadi siku.
Timu hiyo kwa sasa inashika usukani kwenye Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya Real Madrid inayoshika nafasi ya pili na ina rekodi ya kucheza mechi tisa za michuano tofauti bila kupoteza hata moja.
Kwa Xavi ushindi dhidi ya Real Madrid na taji la Super Cup la Hispania ni mambo yanayozidi kumpa heshima na kulinda kibarua chake mbele ya wakurugenzi wa klabu hiyo hasa baada ya timu hiyo kutolewa katka Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Xavi abeba taji la kwanza Barca
Xavi abeba taji la kwanza Barca
Read also