Na mwandishi wetu, mwanza
Boxing Day, Desemba 26 au Siku ya kufungua zawadi imekuwa nzuri kwa mashabiki wa Simba baada ya kupewa zawadi ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Si hilo tu, Simba pia imewapa zawadi ya usajili mpya mashabiki wake ambao wamemshuhudia kwa mara ya kwanza uwanjani kiungo wa zamani wa Yanga, Saido Ntibazonkiza aliyejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Geita Gold ingawa hakucheza mechi hiyo lakini uwapo wake uwanjani ni uthibitisho tosha kwamba sasa ataanza kuvaa jezi ya Simba.
Ushindi huo unaifanya Simba inayoshika nafasi ya pili kufikisha pointi 41 katika michezo 18 ikiwa imeachwa na vinara wa ligi hiyo mahasimu wao Yanga wanaoshika usukani wakiwa na pointi 47 hivyo Simba wana kazi ya kupigania pointi sita za kuifikia Yanga.
Simba iliandika bao la kwanza dakika ya 15 mfungaji akiwa nahodha John Bocco ambaye sasa anakuwa amefikisha mabao sita hivyo ana kazi ya kuwapiku vinara wengine wa mabao wakiongozwa na Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 14, Moses Phiri wa Simba, mabao 10 na Sixtus Sabilo wa Namungo na Idris Mbombo wa Azam wenye mabao saba kila mmoja.
KMC ambao katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo walitoka sare ya mabao 2-2 na Simba, baada ya kufungwa bao na Bocco walitulia na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 52 mfungaji akiwa ni Sadala Lipangile.
Hata hivyo dakika tatu baada ya bao hilo, mambo yalianza kuwaharibikia KMC ambao walijikuta wakifungwa bao la pili mfungaji akiwa ni Augustino Okrah ambaye aliuwahi mpira uliookolewa na kipa wa KMC, David Mapigano.
Beki Henock Inonga alihitimisha mabao ya Simba katika dakika ya 73 akifunga bao kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na mwamba wa Lusaka, Clatous Chama. Kwa Inonga hilo linakuwa bao la pili mfululizo tena akifunga kwa kichwa, alifanya hivyo katika mechi ya mwisho ya Simba dhidi ya Kagera Sugar iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu NBC zilizochezwa Desemba 26, Coastal Union ilitoka sare ya mabao 3-3 na Polisi Tanzania katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.
Soka Simba yawapa zawadi mashabiki
Simba yawapa zawadi mashabiki
Read also