Na mwandishi wetu
Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba imeeleza kuwa kesho Jumamosi itaweka wazi majina ya wagombea waliopita kwenye usaili wa uchaguzi wa viongozi wapya wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Januari, mwakani.
Hayo ni matokeo ya wagombea takriban 23 ambao wamekuwa wakiitwa kwa awamu tangu juzi na kamati hiyo huku baadhi ambao hawakuitwa wameelezwa pia kufahamu hatma yao na sababu zilizopelekea kutofanyiwa usaili huo.
Akizungumza leo Ijumaa jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo, Boniface Lihamwike alisema wanafahamu kumekuwa na maswali na sintofahamu kutoka kwa baadhi ya wagombea wa nyadhifa mbalimbali lakini majibu yote yatayawekwa wazi kesho Jumamosi baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati.
“Tutakachofanya kwa kuwa leo ndiyo tunamaliza usaili, tukishamaliza hilo Jumamosi (kesho) tutatoa majina yote ya ambao wamepita kwenye usaili na pia tutawajulisha watu wote ambao walikuwa hawajapita, tutajua ni njia gani ya kuwajulisha na tutawapa sababu.
“Kusiwe na wasiwasi kwani tukimaliza zoezi hili tutatoa taarifa kwa nini wameitwa na kwa nini wameachwa na walioingia kwenye usaili haimaanishi kwamba wote wanaweza kupita, lakini yote tutayaweka hadharani, wapo ambao hawakuvuka hatua na huo ni utaratibu wa kawaida,” alisema Lihamwike.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, baada ya kuweka majina ya waliopita katika usaili, zoezi litakalofuata ni kupokea na kusikiliza mapingamizi waliyowekewa wagombea, kabla ya kutangaza tena waliopita kwenye awamu hiyo na kisha kuanza rasmi kampeni kuelekea Januari 29, siku ya uchaguzi wenyewe.