Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Meddie Kagere ambaye anaongoza katika orodha ya wafungaji kwenye timu yake amesema lengo lake ni kuweka rekodi ya ufungaji bora kwa mara ya tatu tangu alipokuja hapa nchini.
Kagere ameanza vyema kampeni ya kusaka kiatu cha ufungaji bora akiwa na mabao saba hadi sasa na kuisaidia Singida BS kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi 30.
Akizungumza na GreenSports, Kagere alisema malengo yake ni kuisaidia timu yake kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi kuu, lakini akili na nguvu amezihamishia katika kusaka kiatu cha ufungaji bora ili aweke rekodi ya kuchukua kiatu hicho kwa mara ya tatu akicheza Tanzania.
“Wakati nakuja hapa (Singida) ndoto yangu ilikuwa ni kuisaidia timu yangu kushinda makombe, lakini pia kiu yangu ilikuwa kuwa mfungaji bora jambo nililolifanya mara mbili na hivi sasa nataka kuchukua tena kwa mara ya tatu,” alisema nyota huyo kutoka Rwanda.
“Msimu uliopita sikupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, msimu huu umeanza vizuri na malengo yangu ni kuona nachukua kiatu cha ufungaji na inawezekana kama tutaendelea kushirikiana, huu ni mwanzo tu naamini kuna mengi mazuri yanakuja,” alisema Kagere.
Kagere amejiunga na Singida BS msimu huu akitokea Simba ambako alidumu kwa misimu mitatu na kufanikiwa kuchukua kiatu cha ufungaji bora mara mbili msimu wa 2018/19 alipomaliza na mabao 23 na 2019/20 alipofunga mara 22.
Katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora, Kagere atakuwa na kazi wa kuwapiku kwanza wageni wenzake kwenye ligi hiyo ambao ni Fiston Mayele wa Yanga anayetokea DR Congo anayeshika usukani akiwa na mabao 13 akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.