Madrid, Hispania
Kiungo mkongwe wa Hispania, Andres Iniesta amesema kitendo cha Lionel Messi kushinda taji la Dunia hakiwezi kumaliza mjadala kuhusu mwanasoka bora zaidi wa wakati wote ingawa anaamini Messi tayari ni mwanasoka bora bila hata taji hilo.
Kwa kipindi kirefu, Messi alikuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wanasoka bora wa wakati wote duniani lakini ikaonekana anahitaji kushinda Kombe la Dunia ili awe na hadhi hiyo ambayo wamekuwa wakihusishwa nayo Diego Maradona wa Argentina na Pele wa Brazil.
Iniesta ambaye pia amecheza na Messi katika klabu ya Barcelona kwa takriban miaka 10, amesema mjadala wa Messi kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa wakati wote duniani utaendelea kuwapo hata baada ya Messi kubeba taji la dunia na Argentina. Jumapili iliyopita Argentina ilitwaa taji la dunia kwa kuibwaga Ufaransa kwa penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3 katika dakika 120.
“Kwangu mimi Messi ndiye bora awe na taji la dunia au asiwe nalo,” alisema Iniesta wakati wa uzinduzi wa Capitten football boots, nembo ya viatu ambayo inamilikiwa na kiungo huyo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Vissel Kobe ya Japan
“Nafikiri ukweli kwamba ameshinda taji la dunia, ni sababu tosha ya kuwa na furaha zaidi kwake binafsi tofauti na watu wanavyofikiria, na si kwake tu hata kwa nchi ya Argentina, walikuwa wakipigania hilo na ukweli ni kwamba kwa mazingira ya ubebaji taji hilo yalivyokuwa, inawafanya kuwa na kila sababu za kufurahia,” alisema Iniesta.
“Nina hakika mtu yeyote ambaye hamuoni Messi kuwa ndiye bora duniani atatafuta sababu ya kuendelea kusema hivyo bila kujali ameshinda au hajashinda Kombe la Dunia,” alifafanua Iniesta.
Messi amekuwa akitajwa kuingia katika kundi la Maradona na Pele wanaotajwa kuwa wanasoka bora wa wakati wote lakini huko nyuma wasiokubaliana na hilo wamekuwa wakidai kwamba hawezi kuwa sawa na Pele na Maradona kwa sababu hajabeba Kombe la Dunia.
Baada ya Argentina kubeba Kombe la Dunia ikiwa na Messi, mjadala huo ambao sasa umebatizwa jina la ‘Goat yaani Greatest of All Time’ umeendelea kwa baadhi ya wachambuzi kudai Messi hawezi kuwa kundi moja na Pele aliyeshinda taji la dunia zaidi ya mara moja.