Buenos Aires, Argentina
Jiji la Buenos Aires leo limechangamka, ni siku ya mapumziko, wananchi wanafurahia taji la dunia, wengi wamevaa jezi namba 10 ya Lionel Messi, wanajivunia nahodha wao, wanajivunia ushujaa wa kipa, Emiliano Martinez na timu yao kwa ujumla.
Martinez ambaye pia ni kipa wa klabu ya Aston Villa ya England amefanya kazi kubwa katika mikwaju ya penalti, ubora wake golini ni sababu mojawapo kubwa iliyoiwezesha Argentina kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia baada ya miaka 36.
Ubora wa Martinez ndio uliowafanya mashabiki waliokuwa wakiyaimba majina ya Messi na Kylian Mbappe kabla ya mechi kulazimia kubadili wimbo na kuanza kumtaja na kumjadili kwa namna ambavyo amekuwa msaada kwa timu yake hadi ikatoka na ushindi wa penalti 4-2.
Baada ya mpambano wa nguvu wa dakika 120 zilizoisha kwa sare ya 3-3, hatimaye ikafika zamu ya mikwaju ya penalti, vita ikahamia kwa watu wawili, kipa na mpigaji penalti na kwa namna ya kipekee kipa wa Argentina, Martinez akaibuka shujaa, ndiye aliyewavunja moyo Wafaransa na kuwafanya washindwe kulitetea kombe walilolibeba mwaka 2018 nchini Urusi.
Mbappe alikuwa wa kwanza kupiga penalti ya Ufaransa, bado kidogo Martinez amnyime bao kwa jinsi alivyoufuata mpira lakini ikashindikana. “Ningezuia shuti lake pia, niliruka vibaya lakini kila kitu nilikifanya kwa usahihi.”
Baada ya hapo akaokoa mkwaju wa Kingsley Coman kabla ya kuanza mbwembwe za kucheza golini ambazo inadhaniwa ‘zilimtoa mchezoni’, kiungo Aurelien Tchouameni aliyebeba matumaini makubwa ya Wafaransa lakini akapiga shuti lililotoka nje.
Hadi hapo Martinez akawa shujaa mwingine wa Argentina pengine baada ya Messi, na ingawa Kolo Muani alifunga penalti yake na Ufaransa kupata bao la pili, Argentina wakakamilisha hesabu baada ya Gonzalo Montiel kumalizia penalti ya mwisho iliyozaa bao lililotosha kuandika historia mpya ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni alisema kwamba kabla ya mikwaju ya penalti, Martinez mwenye umri wa miaka 30 sasa aliwaambia wachezaji wenzake anenda kuokoa penalti.
Alipoulizwa kuhusu tukio la penalti lilivyokuwa, Martinez aliyetwaa tuzo ya kipa bora alisema,
“Sina la kusema, nilitulia wakati wa penalti na kila kitu kilienda kama nilivyokuwa nataka, yote yaliyokuwa kwenye ndoto zangu nimeyafanikisha.”