Doha, Qatar
Wakati Neymar akisema hana uhakika wa asilimia 100 kuendelea kuichezea Brazil katika fainali zijazo za Kombe la Dunia, kocha wa timu hiyo, Tite amethibitisha kwamba anang’atuka.
Brazil, moja ya timu iliyopewa nafasi kubwa ya kubeba kombe la Dunia ilitolewa juzi katika hatua ya robo fainali na Croatia kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwa dakika 120.
Akizungumzia uamuzi wake wa kung’atuka kuinoa timu hiyo, Tite mwenye umri wa miaka 61 alisema anakwenda kupumzika baada ya miaka sita ya kuwa kocha wa Brazil lakini Neymar alisema kwamba bado anahitaj kutafakari zaidi kuhusu jambo hilo.
Neymar mwenye umri wa miaka 30 ambaye pia anaichezea klabu ya PSG ya Ufaransa aliifikia rekodi ya mabao 77 ya gwiji wa soka Brazili Pele katika timu ya Taifa akiwa ameichezea timu hiyo jumla ya mechi 124 lakini akashindwa kuibeba mbele ya Croatia.
“Sifungi milango ya kwenye kuichezea timu ya taifa lakini pia siwezi kujihakikishia asilimia 100 kwamba nitarudi katika timu hii,” alisema Neymar ambaye alianza kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18.
Neymar hadi sasa ameichezea Brazil kwenye fainali tatu za Kombe la Dunia, anakumbuka kuiwezesha kufikia hatua ya nusu fainali mwaka 2014 katika fainali ambazo Brazil ilikuwa mwenyeji lakini akaikosa mechi ya nusu fainali dhidi ya Ujerumani baada ya kuumia, mechi ambayo Brazil ilikutana na kichapo cha aibu cha mabao 7-1.
LigiKuu Kocha Brazil ang’atuka
Kocha Brazil ang’atuka
Read also