Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez hana sababu ya kuwa na hofu, anaungwa mkono na Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta licha ya timu hiyo kuyumba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kesho ina mtihani mgumu dhidi ya mahasimu wao Real Madrid katika La Liga.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita Barca ilitoka sare ya mabao 3-3 na Inter Milan na hivyo kujipa matumaini ya uwezekano wa kufuzu hatua ya 16 bora lakini kiujumla timu hiyo bado ina wakati mgumu ikiwa inashika nafasi ya tatu katika kundi lake na haitokuwa ajabu ikiaga michuano hiyo katika hatua ya makundi kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Laporta licha ya kuifahamu hali hiyo na minong’ono iliyoanza kuhusu usajili mkubwa ambao klabu hiyo imeufanya kwa kutumia fedha nyingi, ameendelea kumuunga mkono Xavi akiwataka mashabiki nao wafanye hivyo.
“Ningependa kuwaambia mashabiki kwamba waendelee kuwa na imani, tuna timu nzuri na hilo linatupa furaha, mashabiki wanatakiwa kumuunga mkono Xavi na sisi tutampa sapoti hiyo,” alisema Laporta.
“Xavi ameshaonesha kwamba ni mtu anayeijua klabu hii kisawasawa pamoja na mfumo wake hilo ni mbali na yeye binafsi kuwa mtu mzuri, mambo yatakwenda vizuri na atatupa mafanikio mengi,” alisisitiza Laporta.
“Huwa tunazungumza mara kwa mara, kila baada ya mechi nina utaratibu wa kuzungumza naye, baada ya mechi (ya Jumatano) nilimuona akiwa mnyonge na aliyeumizwa, Xavi ana falsafa ambazo sijaziona kwa mtu mwingine yeyote niliyewahi kukutana naye, wakati wote ana misimamo chanya, ni jambo ambalo wakati wote nimekuwa nikilipenda,” alisema Laporta.

Alisema kwamba tayari amemwambia Xavi aangalie mbele, asiifikirie sana Ligi ya Mabingwa Ulaya na badala yake mtazamo uwe kwenye La Liga ingawa Laporta pia alikiri kwamba kuangukia kwenye Europa Ligi kuna utata wake kwenye masuala ya fedha kwa klabu japo jambo hilo si kubwa sana.
Laporta pia alikiri kwamba kama walivyo watu wengine, yeye pia alikuwa na matumaini makubwa na Barca kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hasa baada ya uwekezaji walioufanya wakati wa dirisha la usajili majira ya kiangazi.
“Sikutarajia hali iwe hivi kwa wakati huu, maofisa katika benchi la ufundi pamoja na kocha wamefanya kila kitu ili timu iwe yenye ushindani, lengo kuu kwa sasa ni La Liga baada ya hali kuwa tete kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini ningependa kulizungumza hilo wakati likiwa limefika mwisho,” alisema.
Barca kwa sasa ndiyo inayoshika usukani katika La Liga ikiwa na pointi 22 sawa na Real Madrid na matokeo ya mechi ya Jumapili ndiyo yatakayoamua kama timu hiyo iendelee kuwa kileleni au iipishe Real Madrid kwenye usukani.
Akiizungumzia mechi hiyo maarufu El Clasico, Laporta alisema, “kwa wakati wote El Clasico ni muhimu kwa sababu yeyote anayeshinda anatokea kuwa na nguvu na kwa anayepoteza anakuwa aliyeathiriwa, matokeo hayo pia yanasaidia kujua nguvu ya mwelekeo wa timu kwamba, tunapoanguka jambo kubwa na la muhimu ni kuinuka, tumedhamiria kubeba La Liga”.