London, Uingereza
Bondia Anthony Joshua amekubali kuzichapa na Tyson Fury ambaye ni bingwa wa ngumi za uzito wa juu duniani anayeshikilia mkanda wa WBC ingawa atalipwa asilimia 40 wakati Fury atalipwa asilimia 60 ya mapato ya pambano hilo.
Promota wa Fury, Eddie Hearn alisema kwamba pambano hilo litafanyika katika Uwanja wa Principality, Cardiff Desemba 17 ingawa awali, Fury alisema kwamba alipanga pambano hilo lifanyike Novemba 26 kwenye Uwanja wa Wembley au Desemba 3 kwenye Uwanja wa Principality lakini ilishindikana.
Uamuzi wa Fury kukubali kuzichapa na Joshua unakuwa ni tofauti na msimamo wake wa awali alipodai kwamba alitaka kuzichapa na Oleksandr Usyk, bingwa wa uzito wa juu anayeshikilia mkanda unaotambuliwa na WBA-IBF-WBO baada ya bondia huyo kumshinda Joshua kwa pointi katika pambano lao la Agosti 20.
Pambano hilo lilishindikana baada ya kutangaza kutoshiriki pambano lolote la ngumi kwa mwaka 2022 na hivyo kumfanya Fury amgeukie Joshua akisema pambano lake na Joshua litaitwa ‘Battle of Britain’ ambapo Joshua alijibu Jumatatu hii akisema kwamba atakuwa tayari kwa pambano hilo.
Akifafanua kuhusu pambano hilo Jumatano hii, Hearn alisema, “Nimewasiliana nao na kuwaambia kwamba tumekubaliana mgao utakuwa ni 60-40 tunataka hilo lirekebishwe katika pambano la marudiano, kwa sababu wewe ndiye bingwa unahitaji mgao mkubwa, jambo ambalo nadhani ni sahihi.
Akizungumzia zaidi kuhusu mgawo huo Fury alisema, “Nafikiri asilimia 60-40 ni zaidi ya uungwana, sikutaka kwenda kuwapa ofa ya asilimia 20 kama ambavyo wangeweza kufanya kwangu badala yake nilikuwa nataka hasa hili pambano liwepo.”
“Tayari nimeshampiga Deontay Wilder na hivyo kuna mtu mmoja na mtu huyo ni AJ (Anthony Joshua) muinua vitu vizito, kwa hiyo ni kwa nini nisimpe asilimia 40 ili asipate sababu na sasa ngoja tuwe na pambano linaloandaliwa kwa ajili ya umma wa Uingereza.
Fury na Joshua ilikuwa wapigane mwaka 2020 baada ya mapromota kudai kwamba thamani ya pambano lao inaweza kufikia Pauni 200 milioni lakini Fury alichukua uamuzi tofauti kwa kuamua kuzichapa na Deontay Wilder wakati Joshua akapanda ulingoni dhidi ya Usyk na kupoteza pambano kwa bondia huyo kutoka Ukraine.
Ngumi Joshua, Fury kuzipiga Desemba
Joshua, Fury kuzipiga Desemba
Read also