Na mwandishi wetu
Simba Queens imewatoa Watanzania kimasomamo kwa kuilaza She Corporate ya Uganda bao 1-0, ushindi uliowapa taji la michuano ya klabu ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) pamoja na kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mafanikio ya Simba Queens yamekuja ikiwa ni takriban miezi miwili baada ya timu ya wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Kwa ushindi huo Simba Queens sasa inajianda kwenda nchini Morocco kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi Novemba mwaka huu wakati Serengeti Girsl itakuwa nchini India Oktoba mwaka huu ikipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo ya dunia.
Katika mechi na She Corporate iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii, Simba Queens walineemeka na bao la mkwaju wa penalti lililojazwa wavuni na Vivian Corazon Aquino dakika chache baada ya mapumziko, penalti iliyotolewa baada ya mchezaji mmoja wa Simba Queens kuangushwa eneo la hatari. Mafanikio ya Simba Queens yalianzia katika mechi za hatua ya makundi baada ya kushinda mechi zote kabla ya kufikia nusu fainali ilipokutana na AS Kigali ya Rwanda na kuichapa mabao 5-1 wakati She Corporate iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Commercial Bank of Ethiopia. Michuano hiyo inayohirikisha klabu za wanawake ukanda wa Cecafa ilianza rasmi mwaka jana ambapo mabingwa walikuwa ni Vihiga Queens kutoka Kenya, timu ambayo haikushiriki michuano ya mwaka huu kwa kuwa Kenya inatumikia adhabu ya kufungiwa na Fifa.
Uamuzi wa Fifa kuifungia Kenya ulichukuliwa baada ya Serikali ya nchi hiyo kumuondoa madarakani na kumpeleka mahakamani aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (KFF), Nick Mwendwa kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za KFF ingawa Mwendwa alishinda kesi hiyo na sasa yuko huru.