New York, Marekani
Msanii wa pop, Britney Spears amesema kwamba ataendelea kuteswa na matukio yake ya miaka ya nyuma ikiwamo ulevi na kila aina ya anasa na anaamini hakuna namna ya kumaliza hali hiyo labda iwe ni kwa njia ya miujiza.
Britney ameendelea kufunguka kuhusu maisha yake ya nyuma ambapo kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo ameelezea ni kwa vipi kuna mambo ambayo hayawezi kumsahaulisha matukio yake ya miaka ya nyuma na kwa nini aliamua kutupia picha na video zake kwenye mitandao huku akidai kwamba anaamini sasa ana muonekano mzuri.
“Kila mtu maisha yake yanaonekana yako sawa, na ninapotupia picha na habari mitandaoni nafikiri kwa muda mwingi, huwa nateswa na kusumbuliwa na maisha yangu ya siku za nyuma, nani anayeweza kusahau mambo ya siku za nyuma, ndio najaribu kutupia picha zangu nikiwa katika muonekano mzuri au kile kinachoonekana kuwa ni maisha mazuri,” alisema Britney.
“Ni kweli sasa niko vizuri kifikra lakini nitaendelea kuteswa na uzoefu wa maisha yangu ya siku za nyuma, sina namna ya kutatua hilo fikra zangu zinateswa na jambo hilo, nafikiri nitahitaji miujiza ya kumaliza jambo hili,” alisema msanii huyo mwenye umri wa miaka 40 sasa na kuongeza kwamba hadi sasa huwa analia peke yake wakati akilala na huwa anakosa amani.
Britney akiwa mwenye mafanikio katika muziki hasa miaka ya 2000 mwishoni aliingia katika utumiaji madawa ya kulevya na anasa za kila aina hadi akawekewa zuio na mahakama kwa takriban miaka 13 ikiwamo kuzuiwa kulea watoto wake, kuanzisha familia mpya na kunyimwa usimamizi wa fedha zake, mmoja wa wasimamizi aliyepewa jukumu na mahakama akiwa ni baba yake, Jamie Spears.
Jamie Spears na wasimamizi wengine hata hivyo inadaiwa sasa wanachunguzwa kwa amri ya mahakama akidaiwa kukiuka taratibu za usimamizi wa msanii huyo.
Tangu mahakama ifute zuio hilo Novemba mwaka jana na Britney kupewa uhuru kujiamulia mambo yake mwenyewe, msanii huyo alifunga ndoa na rafiki yake wa zamani, Sam Asghari na pia akishirikiana na wasanii wengine anajiandaa kukipika upya kibao cha mwanamuziki Elton John cha ‘Tiny Dancer’ alichokitoa mwaka 1972 ambacho huenda Ijumaa kikatoka.
Hollywood Britney Spears ateswa na maisha ya anasa
Britney Spears ateswa na maisha ya anasa
Related posts
Read also