London, England
Bilionea maarufu wa London, Sir Jim Ratcliffe anadaiwa kutaka kununua hisa katika klabu ya Manchester United.
Sir Jim mwenye umri wa miaka 69, anatajwa kuwa mmoja wa watu matajiri wa Uingereza kwa mujibu wa takwimu zilizowahi kutolewa na Jarida la Forbes.
“Kama klabu inauzwa hapana shaka Jim atakuwa mmoja wa watu wenye uwezekano wa kununua hisa, kama jambo hili linawezekana tutapenda kufanya mazungumzo lengo likiwa ni kuwa na umiliki wa muda mrefu,” alisema msemaji wa bilionea huyo.
Swali ambalo hata hivyo linaendelea kutatiza wengi ni kuhusu familia ya Glazer kama itakuwa tayari kuuza hisa nyingi za klabu hiyo ingawa kumekuwapo habari kwamba mpango huo upo.
Man Utd, moja ya klabu zilizowahi kutamba katika Ligi Kuu England ikiwa na rekodi ya kulitwaa taji la ligi hiyo mara 20, kwa sasa mambo yake hayako vizuri na wakiwa chini ya kocha wao mpya, Erik ten Hag, tayari wamepoteza mechi mbili za awali za msimu mpya wa 2022/23.
Tayari kumeshaanza kuibuka shutuma dhidi ya familia ya Glazer ambayo inalalamikiwa kwa kutokuwa tayari kuwekeza katika timu hali inayoaminika kuwa kikwazo cha mafanikio ikiwamo suala zima la usajili ambapo timu hiyo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikimtaka kiungo wa Barcelona, Frankie de Jong lakini usajili huo umekuwa mgumu kukamilika.
Mashabiki wa Man Utd kupitia Manchester United Suppoters Trust (MUST), wameipokea kwa mikono miwili habari ya Jim kuhusishwa na uwekezaji katika klabu hiyo. “Hili si suala la fedha zilizotumika au la, Jim anaangalia nini kinaweza kufanyika kwa wakati huu, na anafahamu ni kwa kiasi gani klabu hii ni muhimu kwa jiji la Manchester, inaonekana kama huu ni wakati sahihi wa kuweka mambo sawa,” alisema msemaji wa MUST.
Jim anayeaminika kuwa ni shabiki wa Man Utd, alishindwa kuinunua Chelsea baada ya mmiliki wake, Roman Abramovich kutangaza kuipiga bei kwa ofa iliyotajwa kufikia Pauni 4.25 bilioni lakini alisema kwamba hakutangaza nia ya kutaka kuinunua Man Utd kwa sababu wakati huo Man Utd haikuwa na mpango wowote wa kuuza hisa zake.
Kimataifa Bilionea London kuinunua Man Utd
Bilionea London kuinunua Man Utd
Read also