Na mwandishi wetu
Mwanzo mzuri kwa Simba, mwanzo mbaya kwa Geita Gold baada ya kulala kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya timu hizo ya Ligi Kuu ya NBC iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Alikuwa ni Augustine Okrah aliyefungua ukurasa wa mabao kwa timu ya Simba alipoandika bao la kwanza katika dakika ya 36 kwa shuti la mguu wa kushoto akiutumia mpira wa adhabu nje kidogo ya 18 baada ya Clatous Chama kuchezewa rafu na timu hizo kwenda mapumziko, Simba ikiwa mbele.
Simba waliandika bao la pili katika dakika ya 56 lililofungwa na Moses Phiri, bao lililoanzia na mpira mrefu uliopigwa na Peter Banda na kumkuta Chama aliyemuuunganishia mfungaji ambaye aliujaza mpira wavuni akiwa karibu na lango la Geita.
Zikiwa zimebakia dakika 10 mpira kumalizika Kelvin Nashon wa Geita alimchezea rafu, Okrah ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuipa Simba penalti ambayo ilijazwa wavuni na Chama na kuifanya Simba itoke uwanjani na pointi tatu na mabao matatu muhimu.
Matokeo hayo yaliyopatikana ligi ikiwa ndio kwanza mbichi, yanaifanya Simba kuwapiku mahasimu wao Yanga pamoja na Mbeya City, timu ambazo pia zimeianza ligi kwa ushindi, Mbeya City ikiilaza Dodoma Jiji mabao 3-1 wakati Yanga iliilaza Polisi Tanzania kwa mabao 2-1.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Azam nayo imeianza ligi kwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kuilaza Kagera Sugar kwa mabao 2-1 wakati Coastal Union ikiwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha nayo imeilaza KMC kwa bao 1-0.
Kwa matokeo ya mechi hizo, Simba ndiyo inayoshika usukani wa ligi hadi sasa ikiwa na pointi tatu na mabao matatu ikifuatiwa na Mbeya City ambayo pia ina pointi tatu na mabao matatu lakini imefungwa bao moja hali inayoitofautisha na Simba ambayo haijafungwa bao hata moja. Azam na Yanga zinashika nafasi ya tatu na nne zikiwa zimefungana kwa kila kitu, zote zimeanza ligi kwa ushindi wa mabao 2-1.
.
Soka Simba yaisulubu Geita, Azam yatamba
Simba yaisulubu Geita, Azam yatamba
Read also