Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Namungo, Reliants Lusajo ni kama vile ameanza mapema mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2022/23 baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
Lusajo amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili kwenye mechi moja msimu huu katika sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mchezaji huyo msimu uliopita alikuwa akipigana vikumbo kwenye kuwania kiatu cha ufungaji bora kilichotua kwa George Mpole wa Geita Gold aliyefunga mabao 17 dhidi ya Fiston Mayele aliyefunga mabao 16 huku Lusajo akimaliza wa tatu kwa mabao yake 10.
Pamoja ya kuanza vyema msimu huu lakini Lusajo amejiweka kando katika mbio hizo akidai jukumu lake la kwanza ni kuisaidia timu hiyo pekee hivyo hata akiwa anafunga hapigi hesabu zake binafsi zaidi ya hesabu za kuisaidia timu kwanza.
“Nashukuru Mungu kwa kufunga mabao hayo mawili lakini kwangu kikubwa ninachokiangalia zaidi ni timu yetu kufanya vizuri, siyo mimi binafsi ingawa ni muhimu lakini zaidi tunaangalia timu sio mtu mmoja mmoja.
“Ndiyo maana nasema nimejiandaa vizuri kwa ajili ya timu, ndiyo iliyotuweka hapa na ndiyo tunayoipambania, ninaamini tutaendelea kujitoa na kufanya vizuri kwa ajili ya timu kwanza,” alisema Lusajo mshambuliaji wa zamani wa Yanga.
Msimu uliopita wa 2021/22, Lusajo alionyesha matumaini katika kuwania tuzo ya mfungaji bora lakini kadri ligi ilivyokuwa ikienda kasi yake ilianza kupungua na akawaacha Mayele na Mpole wakichuana kabla ya Mpole kuibuka kinara.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Ihefu ilishindwa kutamba nyumbani baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya Ruvu Shooting.
Soka Lusajo aanza mbio ufungaji bora
Lusajo aanza mbio ufungaji bora
Read also