Na mwandishi wetu
Beki wa Crystal Palace, Joachim Andersen amesema kwamba ametishiwa kuuawa yeye na familia yake baada ya kupigwa kichwa na mchezaji wa Liverpool, Darwin Nunez katika mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa jana kwenye dimba la Anfield na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Nunez alipewa kadi nyekundu hapo hapo baada ya kumpiga kichwa Andersen katika kipindi cha pili wenyeji Liverpool wakiwa nyuma kwa bao moja lililofungwa na Wilfried Zaha.
Liverpool hata hivyo ilifanikiwa kunusuru pointi kwa bao la Luis Dias lakini matokeo hayo yanaifanya timu hiyo iwe imecheza mechi yake ya pili ya Ligi Kuu England ikiwa haina ushindi hata mmoja jambo ambalo linaonekana kuwakera mashabiki ambao wameelekeza hasira zao kwa Anderson kupitia mtandao wa Instagram kwa kumtumia ujumbe wa kumtisha.
“Nimepata ujumbe mara 300 hadi 400 usiku, naelewa mnaishabikia timu lakini muwe na heshima na acheni kunitumia ujumbe mkali,” alisema Anderson kabla ya kuonyesha baadhi ya ujumbe aliokuwa akitumiwa ikiwamo shutuma na kutishiwa kifo na kuongeza kwamba anaamini maofisa wa Instagram na wale wa Ligi Kuu England watachukua hatua..
Wakati huo huo beki wa Liverpool, Virgil van Dijk amemshauri Nunez kujifunza kutokana na makosa yake baada ya kupewa kadi nyekundu na kutoka nje kwa kosa la kumpiga mchezaji mwenzake kichwa katika mechi yake ya kwanza ya nyumbani Anfield.
“Ni lazima awe mwenye kujizuia, ni lazima ajitathmini, ni lazima afahamu kwamba haya mambo hutokea hasa katika Ligi Kuu, hilo linatakiwa kuwa somo kwake na naamini jambo hilo halitotokea tena, ni wazi kwamba alivurugwa,” alisema Van Dijk.
Nunez ambaye alijiunga na Liverpool akitokea Benfica ya Ureno kwa ada ya Euro 75 milioni sasa atalazimika kukosa mechi tatu ikiwamo mechi ya Liverpool dhidi ya mahasimu wao Manchester United wiki ijayo.
Kimataifa Beki England atishiwa kifo
Beki England atishiwa kifo
Related posts
Read also