Na Hassan Kingu
Haji Manara akiwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miaka miwili kutojihusisha na masuala ya soka, ameacha maswali yanayoonekana kuwa ya kisheria baada ya kushiriki tamasha la Wiki ya Mwananchi lakini akijitambulisha kwa jina la MC kutoka Kigogo, Sambusa, Dar es Salaam. Je nini hatma yake?
Ikitokea akapewa nafasi ya kujitetea mbele ya Kamati ya Maadili ya TFF, iwe ni yeye au kwa msaada wa wakili wake, Manara atapenda zaidi kujitambulisha kwa kazi yake ya U-MC kutoka Kigogo kuwa ndiyo iliyompelaka uwanjani, hatotaka kujihusisha na usemaji wa Yanga, atajitenga kwa nguvu zote na soka, hapo ndipo utetezi wake utakapopata nguvu.
Wakili au Manara katika kujitetea kwake atasema tu kwamba nimefungiwa kushiriki masuala ya soka lakini sijafungiwa kufanya kazi ya U-MC, hapo ndipo utetezi wake utakaposimamia, atatoa ufafanuzi mwingi sana katika kutetea hoja yake hiyo.
Atafafanua kwamba angeweza kwenda uwanjani siku ya Wiki ya Mwananchi na kufanya biashara ya kuuza maji au ice cream na kujitetea kwamba kamati ya TFF haina mamlaka ya kumsimamisha katika shughuli za kibiashara, angeweza hata kuingia na gari la wagonjwa na kuwahudumia wachezaji wa Yanga, kamati hiyo pia isingeweza kumzuia kwa kuwa haina mamlaka katika mambo hayo.
Angeingia na gari la Yanga kwa kibali cha udereva na kujitetea kwamba kamati ya TFF haihusiki na kazi hiyo hasa kwa kuwa yeye ana leseni ya udereva na yeye udereva ni kazi yake, wenye mamlaka ya kumzuia kufanya kazi hiyo ni askari si TFF.
Angeweza kuingia uwanjani na kundi lolote binafsi la burudani kwa madai kwamba yeye ni mmoja wa wasanii wa kundi hilo, akaimba na kuisifia Yanga kwa namna ya kipekee na kushangiliwa na mashabiki, bado kisheria kamati ya TFF isingekuwa na mamlaka ya kumuingilia katika hilo au kumzuia asishiriki katika kikundi cha muziki ambacho kimekodiwa na kulipwa na Yanga na yeye anapata kula yake kupitia kikundi hicho.
Angeweza kujihusisha na tukio la Wiki ya Mwananchi kama mwandishi wa habari, akakaa studio ya kituo cha televisheni au redio na kufanya kazi ya kuripoti mpira, TFF ikimhoji atawaambia katumwa na bosi wake kuripoti mechi na bosi wake hapangiwi mtu wa kumtuma kazini na TFF, anaangalia waandishi alionao na wenye sifa za kukipendezesha kipindi.
Katika kuonyesha Manara amefanya kosa upande wa TFF nao watakuwa na kazi ya kuonyesha kwamba Manara kakosa na hivyo anahitaji kuongezewa adhabu yeye pamoja na Rais wa Yanga, Hersi Saidi,
Wakili au mwanasheria wa upande wa TFF atamhoji na hapa najaribu tu kujipa picha ya namna mahojiano yenyewe yanavyoweza kuwa…
Wakili: Jina lako nani?
Manara: Haji Manara
Wakili: Unafanya kazi gani?
Manara: MC kutoka Kigogo Sambusa (hapa Manara atajitahidi kujitenga na Yanga)
Wakili: Unaijua TFF ni kitu gani?
Manara: Ndio, ni Shirikisho la Soka Tanzania
Wakili: Umewahi kuadhibiwa na TFF?
Manara: Ndio, nimefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka miwili ndani na nje ya nchi
Wakili: Unakumbuka Agosti 6 mwaka huu mida ya saa 10 ulikuwa maeneo gani?
Ndio: Uwanja wa Mkapa
Wakili: Kulikua na nini hapo Uwanja wa Mkapa?
Manara: Matukio ya burudani mbalimbali
Wakili: Unaweza kuyataja matukio hayo?
Manara: Kulikuwa na burudani ya muziki, pia kulikuwa na mechi ya soka baina ya Yanga na St George
Wakili: Kwa hiyo ulishiriki tukio linalohusisha soka wakati umekiri kufungiwa
Manara: Ndio nilishiriki lakini nilishiriki kama MC
Wakili: Sijakuuliza ulishiriki kama nani nataka kujua kama ulishiriki
Manara: Ndio nilishiriki lakini kazi yangu ilikuwa ni kufanya utambulisho tu haihusiani na soka
Wakili: Utambulisho wa kina nani?
Manara: Utambulisho wa wanasoka wapya wa Yanga
Wakili: Kwa hiyo tukisema ulishiriki tukio linalohusu soka tutakuwa sahihi?
Wakili: Hapana mimi kazi yangu ilikuwa kutambulisha wachezaji tu, nilipewa kazi hiyo kama MC kutoka Kigogo Sambusa.
Wakili: Sina swali jingine.
Baada ya hapo sasa hukumu itatolewa, hapo inategemea zaidi busara za mtoa hukumu na uwezekano wa Manara kushinda ni jambo linalowezekana.
Nimetoa mfano huu kwa sababu ya imani niliyonayo kwamba wengi wa mashabiki wa soka wanaamini katika mazingira ya aina hiyo, wapo ambao wanaamini kwa asilimia 100 kwamba Manara anaibuka mshindi kwa hatua yake ya kwenda uwanjani kama MC, kwa maana ya kwamba amepewa kazi ambayo asingeweza kuikataa.
Mtazamo huu unabebwa na fikra kwamba Manara atakuwa akijitetea katika mahakama za kiraia na si zile za soka, katika mahakama za soka mara nyingi huendeshwa na watu wanaoitwa benevolent dictators yaani madikteta wasio wababe au madikteta waungwana (tafsiri yangu), si watu wa kumtia mtu ndani au kumpa mateso bali uamuzi wao ni wa mwisho na hauhusishi kuteswa au kupigwa.
Hawataki kupingwa kwenye mahakama za kiraia, ukitaka kuupinga uamuzi wao, utatakiwa kuupinga katika mfumo huo huo wa kisoka ambao ni mgumu kushinda, ukienda nje ya hapo utajitafutia matatizo, jirani zetu Kenya wameingia kwenye matatizo kwa sababu tu ya kutaka kumshughulikia mhalifu kwa mfumo wa kiserikali na si kisoka.
Rais wa Shirikisho la Soka Kenya kakutwa na hatia ya matumizi mabaya ya fedha, serikali ikamfikisha kwenye mahakama za kiraia, kwa hofu kwamba akiendelea kuwa madarakani atavuruga ushahidi, ikampora madaraka yake ndani ya shirikisho, kosa likaanzia hapo, madikteta waungwana wakaingilia kati na kuhoji kwa nini mmempora madaraka yake, Kenya leo hii imefungiwa kushiriki Afcon.
Kwa hiyo sitashangaa nikisikia adhabu ya Manara ikibaki vile vile kwa kuwa aliwahi kuomba msamaha huko nyuma au hata kuongezwa, lakini pia sitoshangaa nikisikia rais wa Yanga, Hersi naye akiadhibiwa iwe ni kwa faini au hata kufungiwa,
Hukumu za kimpira zitamuangalia Manara aliyekuwapo kwenye tukio la Wiki ya Mwananchi na kuishia hapo, hoja za MC wa Kigogo Sambusa kwao hazitokuwa na nafasi, nafasi hiyo ataipata tu kwenye mahakama za kiraia, si zile za soka, kwa hiyo Manara anaweza akajikuta akihukumiwa tena kwa kutotii masharti ya adhabu, Hersi naye anaweza akajikuta akihukumiwa kwa kumpa nafasi mtu aliyeadhibiwa na TFF. Tusubiri.
Soka Nini hatma ya MC wa Kigogo Sambusa?
Nini hatma ya MC wa Kigogo Sambusa?
Related posts
Read also