Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Minziro ameeleza hofu aliyonayo juu ya kuchelewa kuongeza mkataba mpya kuinoa timu hiyo namna inavyoweza kumkwamisha kwenye michuano watakayoshiriki msimu ujao.
Imeelezwa kuwa leo au kesho ilitarajiwa kukamilika kwa dili hilo ambalo limechelewa kutokana na sababu mbalimbali ambazo Minziro hakutaka kuziweka wazi akidai ni majadiliano ya kimkataba.
Minziro aliyeipandisha timu hiyo kushiriki Ligi Kuu Bara mara ya kwanza msimu uliopita alisema kwa sasa yupo mbali na maandalizi ya timu mpaka amalizane na uongozi, ingawa benchi la ufundi linaendelea na kazi lakini bado haileti afya ya maandalizi ya timu.
“Ni kweli ligi inaanza wiki ijayo tu hapo, maandalizi yanaendelea lakini hasa nilihitaji kuwa na mechi hasa za kirafiki kuona mapungufu mapema lakini ni kama tumechelewa kwa sababu bado sijamalizana na uongozi juu ya mkataba.
“Pengine leo au kesho naweza nikaenda Geita kumaliza hilo maana hata leo tumewasiliana, mazungumzo yanakwenda vizuri lakini wasiwasi ni muda wa maandalizi ya timu na michuano tuliyonayo msimu ujao,” alisema Minziro kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga.
Geita iliyomaliza nafasi ya nne msimu uliopita, msimu ujao mbali na michuano ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA lakini pia watakuwa na kibarua kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitarajia kuanza hatua ya awali dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan.
Katika mechi hizo za hatua ya awali, Geita itaanzia ugenini Septemba 9 kabla ya kurudiana kwenye mchezo watakaokuwa nyumbani mnamo Septemba 16, mwaka huu.
Soka Mkataba wa Minziro Geita wachelewa
Mkataba wa Minziro Geita wachelewa
Read also