New York, Marekani
Nyota wa mchezo wa tenisi duniani, Serena Williams ametoa kauli inayoashiria kujiandaa kustaafu mchezo huo licha ya kutokuwa wazi na kusema kwamba baada ya Mashindano ya Wazi ya Marekani (US Open) atajitenga kidogo na mchezo huo.
Akiandika katika Jarida la Vogue, Serena mwenye umri wa miaka 40 sasa na kinara wa Grand Slam mara 23 alisema kwamba anajipanga kwenda kufanya mambo mengine muhimu na kwamba safari hiyo inaanza hapo hapo akasema kwamba halipendi neno kustaafu.
Juni mwaka huu Serena aliibukia kwenye michuano ya tenisi ya Wimbledon baada ya kuwa nje kwa kipindi kirefu akiandamwa na majeraha, alisema kwamba atashiriki katika Mashindano ya Wazi ya Marekani akiwa na rekodi ya kushinda mashindano hayo kwa mtu mmoja mmoja mataji sita kuliko mcheza tenisi mwanamke yeyote na akishika nafasi ya pili kwa rekodi ya jumla ya mashindano hayo akiwa ametanguliwa na Margaret Court.
“Bahati mbaya sikuweza kushinda Michezo ya Wimbledon mwaka huu na sijui kama nitakuwa tayari kushinda ile ya New York lakini nitajaribu,” alisema.
“Najua kuna hamasa kutoka kwa mashabiki kwamba ningeweza kuifikia rekodi ya Margaret siku ile London, na labda kuipiku rekodi hiyo New York, na baada ya hapo kupewa taji na kufanya sherehe, nalijua hilo, ni hamasa nzuri ingawa siangalii hilo,” alisema.
“Ninapata tabu sana kuaga, ni jambo baya duniani lakini tafadhali eleweni kwamba ninawashukuru katika namna ambayo siwezi kuieleza kwa maneno,” aliongeza.
Serena alisema kwamba amekuwa akisita yeye mwenyewe kujiambia au kumwambia mtu mwingine yeyote kwamba analazimika kujiweka kando na tenisi.
“Ni jambo gumu, Alexis, mume wangu na mimi hatukuwahi kuzungumza hili, ni kama mada haramu, pia siwezi hata kuwa na mazungumzo ya aina hii na mama au baba, najikuta katika wakati mgumu, koo linakwama na najikuta nikianza kulia, kuna watu wengi nawajua ambao hufurahia kulizungumza hili na wako tayari kulipokea, natamani nami ningekuwa katika hali kama hiyo,” alisema.
Kutokana na mafanikio yao kwenye mchezo wa tenisi, Serena na dada yake, Venus wanatajwa kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mchezo huo kwa kuuongezea umaarufu duniani ikiwamo kutoa hamasa kwa wachezaji wa baadaye huku pia wakidaiwa kuwa mstari wa mbele kwenye kutetea masuala ya haki za kijinsia.
Sports Mix Serena Williams kustaafu tenisi
Serena Williams kustaafu tenisi
Read also