Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema amesema kwamba timu hiyo haihitaji kusajili straika namba 9 kwa kuwa tayari ina wachezaji wengine wanaomudu nafasi hiyo.
Benzema, amekuwa na msimu wenye mafanikio wa 2021/22 akiiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Spanish Super Cup huku akifunga jumla ya mabao 44 katika mechi 46 za michuano mbalimbali.
Madrid tayari imemsajili kiungo Aurelien Tchouameni kutoka Monaco na beki wa kati Antonio Rudiger aliyetokea Chelsea lakini ilishindwa kuinasa saini ya mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe ambaye iliaminika kuwa angesaidia kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
“Kuna wachezaji wengi hapa ambao wanaweza kucheza namba 9 kwa sababu hapa Real Madrid mshambuliaji hawi tu namba 9 ambaye anasubiri kuletewa mipira, ni lazima uzunguke kote,” alisema Benzema leo wakati timu yake jioni hii ikijiandaa kuumana na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani katika mechi ya kuwania taji la Uefa Supercup.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti naye alisema wana wachezaji wengi na kumtolea mfano Eden Hazard aliyesema ana uwezo wa kucheza namba tisa feki kama Benzema hatokuwapo. “Tunao wengi, orodha ni nzuri Karim, Mariano, Hazard, Rodrygo, Vinicius, Asensio japo ni kweli kwamba unapomkosa mshambuliaji bora duniani (Benzema) hiyo inaiathiri timu lakini suluhisho tunalo,” alisema Ancelloti.
Benzema pia alizungumzia tuzo ya Ballon d’Or na nafasi ya yeye kuibeba tuzo hiyo au atakuwa mwenye furaha iwapo kipa wao, Thibaut Courtois ataibuka mshindi wa tuzo hiyo, “Thibaut Courtois kwangu ni kipa bora duniani, kuwe na Ballon d’Or au kusiwe na Ballon d’Or, hilo ndilo ninaloweza kulisema.”
Kimataifa Benzema: Madrid haihitaji straika
Benzema: Madrid haihitaji straika
Read also