Na mwandishi wetu
Mashabiki wa Yanga leo wametoka vichwa chini katika Siku ya Mwananchi baada ya timu yao kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Vipers ya Uganda katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ni mtihani wa kwanza mgumu kwa Yanga tangu kumalizika kwa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2021/22 na hivyo matokeo yanabaki kuwa somo zuri kwa benchi la ufundi la Yanga kujua nini cha kurekebisha kabla ya timu hiyo kuanza kulitetea taji la ligi wanalolishikilia.
Vipers ambao ni vinara wa Ligi Kuu Uganda waliwashitukiza Yanga kwa bao la dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, bao ambalo lilifungwa na Milton Karisa na ingawa bao hilo halikuwateteresha Yanga ambao mara kwa mara walikuwa wakishangiliwa na mashabiki wao waliojanza uwanjani, bado hawakuweza kuipenya ngome ya Vipers.
Dakika 20 baada ya kuanza kipindi cha pili, Yanga walijikuta wakipachikwa bao la pili ambalo mfungaji, Anukani Bright alifunga bao hilo kwa shuti la kona iliyokwenda moja kwa moja hadi wavuni na kuwaacha mashabiki wa Yanga wakiwa wameduwaa wasiamini kilichotokea.
Yanga baada ya kuona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, kipindi cha pili iliwaingiza mastaa wake wapya waliosajiliwa kwa mbwembwe kina Joyce Lomalisa, Stephen Aziz Ki, Bernard Morrison na Gael Bigirimana ambao hata hivyo hawakuweza kubadili matokeo.
Yanga baada ya mechi hiyo sasa wanajiandaa na Ligi Kuu ya NBC ingawa kabla ya kuanza mbio hizo, Jumamosi ijayo watakuwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya mahasimu wao Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo pia itakuwa kama uzinduzi wa msimu mpya wa 2022/23.
Soka Vipers waivuruga Siku ya Mwananchi
Vipers waivuruga Siku ya Mwananchi
Read also