London, England
Habari ya Cristiano Ronaldo kutocheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England huenda ikabadilika baada ya kuumia kwa Anthony Martial na hivyo kumfanya kocha Erik ten Hag kubadili msimamo na kumpa nafasi mchezaji huyo.
Man United itaanza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England Jumapili hii dhidi ya Brighton, mechi ambayo tayari ilishaelezwa kwamba Ten Hag alishaamua kutompa nafasi Ronaldo ambaye tangu kumalizika msimu wa 2021/22 hakuonekana katika timu hiyo kwa kilichodaiwa kuwa ni matatizo ya kifamilia ingawa inadhaniwa kuwa ni mgomo baridi wa kushinikiza kuondoka.
Man United imefanya ziara ya takriban wiki mbili katika nchi za Thailand na Australia na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo Ronaldo hakushiriki kabla ya kujitokeza Jumapili iliyopita katika mechi nyingine ya kirafiki na Rayo Vallecano iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, mechi ambayo alicheza dakika 45 za mwanzo kabla ya kutolewa lakini akaondoka uwanjani zikiwa zimebakia dakika 10 mpira kumalizika.
Matukio yote hayo hayajamfurahisha Ten Hag ambaye inadaiwa ameamua kutompa nafasi katika mechi na Brighton japo amedai kwamba mchezaji huyo hayuko fiti lakini kuumia kwa Martial kunamfanya Ten Hag afikirie upya ama kumpa nafasi Ronaldo au kuja na mpango mwingine.
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Martial na ilionekana kama maisha yake ya soka Man Utd yalikuwa yakielekea ukingoni lakini ameonyesha kuja na ari mpya katika mechi za kirafiki za hivi karibuni ingawa wako wanaodhani kuwa kukosekana kwa Ronaldo ni sababu mojawapo ya nyota ya Martial kung’ara katika mechi hizo.
Juhudi za Martial zimemfanya Ten Hag kumkubali mchezaji huyo na kuanza kumpigia hesabu kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo katika msimu wa 2022/23 hasa akiamini anaweza kucheza vizuri nafasi ya winga na hivyo kumuweka benchi Ronaldo lisingekuwa jambo kubwa.
Martial hata hivyo kwa sasa anasumbuliwa na misuli baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Atletico Madrid mjini Oslo, Norway na sasa anatarajia kuwa nje akijiuguza kwa kipindi cha siku tano hadi 10 na hapo ndipo nafasi ya Ronaldo inapoanza kujadiliwa na wachambuzi wakijiuliza kuhusu atakachofanya Ten Hag ili kuwa na mtu mzoefu kikosini hasa katika safu ya ushambuliaji.
Na ingawa Ten Hag ameshasema kwamba Ronaldo hayuko fiti lakini sasa huenda akalazimika kumuingiza katika hesabu zake au kumpa nafasi hiyo Marcus Rashford au kuja na mpango mwingine hapo Jumapili.
Kimataifa Ten Hag kumpanga Ronaldo Jpili?
Ten Hag kumpanga Ronaldo Jpili?
Read also