Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans van Der Pluijm ametahadharisha mapema kuwa atahakikisha anapambana na timu kubwa za Ligi Kuu ya NBC ili kuonesha ushindani na ubora wao msimu ujao.
Pluijm raia wa Uholanzi amefunguka hayo baada ya kuridhishwa na kiwango cha timu yake ilipoumana na Zanaco ya Zambia jana na kushinda kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Liti (zamani Namfua), Singida.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Yanga na Azam amesema kwamba kiufundi bado anahitaji kurekebisha kikosi hicho sehemu kadhaa ili kuwa tishio zaidi na kuwaletea changamoto ya ushindani vigogo wanaoshika nafasi za juu kila msimu ambao ni Simba, Yanga na Azam ili kufanya vyema msimu ujao.
“Mchezo wetu na Zanaco ulikuwa mgumu na fursa nzuri ya kujifunza zaidi, tumeona kuna baadhi ya idara inabidi kuziweka sawa na kurekebisha suala la mawasiliano uwanjani ambalo ni muhimu sana.
“Unajua mpira hautabiriki lakini tunataka kuleta changamoto ya ushindani kwa timu kubwa, natumani tutafanya hivyo, pia tunatakiwa kushinda mechi hizi nyingine si tu kushinda kubwa, suala ambalo litategemea nguvu kazi na utayari wa wachezaji na kiubora nafikiri tuna asilimia 67, tunatafuta 30 za kukaa sawa kabisa,” alisema Pluijm.
Singida iliyokuwa ikiitwa DTB iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao wa 2022/23 imekuwa gumzo kutokana na usajili wa wachezaji wenye majina wanaoendelea kuufanya na kutabiriwa kuleta changmoto kubwa msimu ujao.
Baadhi ya wachezaji waliotambulishwa na Singida mpaka sasa ni Deus Kaseke, Paul Godfrey, Yassin Mustapha kutoka Yanga, Meddie Kegere, Pascal Wawa, Said Ndemla waliokuwa Simba, Kelvin Sabato aliyekuwa Mtibwa Sugar, kipa Metacha Mnata aliyetoka Polisi Tanzania na wengine wengi.
Soka Pluijm aahidi ushindani Ligi Kuu
Pluijm aahidi ushindani Ligi Kuu
Read also