Na mwandishi wetu
Timu ya Singida Big Stars imetangaza kuingia mkataba wa miaka minne na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya Sportpesa kama mdhamini wao mkuu.
Hatua hiyo ya Sportpesa imekuja ikiwa ni wiki moja imepita tangu watangaze kuingia mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh 12.3 bilioni ingawa upande wa Singida hawakutaka kuweka wazi thamani ya mkataba huo.
Kampuni hiyo imeingia mkataba na Singida baada ya kuachana na Simba waliokuwa wakiwadhamini pia misimu ya nyuma ambao wao wameingia mkataba mpya na Kampuni ya M-Bet.
Akizungumza na GreenSports, Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa Singida Big, Muhibu Kanu alisema kutokuweka wazi thamani ya mkataba huo ni makubaliano ya pande zote mbili, akidai hilo siyo la msingi sana kwa sasa zaidi ya kuhakikisha fedha walizopata zinainufaisha timu.
“Tunashukuru kuingia mkataba huu na Sportpesa wakiwa na nafasi ya kutangaza kupitia hapa, nasi tukifurahi kupata fursa hii itakayotusaidia mno kuendesha timu katika misimu hiyo, cha muhimu zaidi ni kuona Wanasingida wanafurahi na timu inapata matokeo mazuri.
“Bado kumekuwa na mazungumzo na kampuni nyingine kuelekea kwenye udhamini wa Singida, nafikiri kesho tunaweza kuwa na matangazo mengine mapya ya kushtukiza kuhusiana na udhamini kwenye tamasha letu la Singida Big Day,” alisema Kanu.
Tamasha hilo litakalokwenda sambamba na utambulisho wa wachezaji wao wapya linatarajia kufanyika Uwanja wa Liti, Singida. Singida Big zamani DTB imepanda kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2022/23 utakaoanza rasmi Agosti 17 mwaka huu.
Soka Sportpesa mdhamini mpya Singida Big
Sportpesa mdhamini mpya Singida Big
Read also