Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Azam umefunguka kuwa haikuwa matakwa yao kuachana na kiungo wao, Mudathir Yahya isipokuwa mchezaji huyo aligoma kusaini mkataba mpya na klabu hiyo.
Jana Azam ilitangaza kuachana na Mudathir na kuibua hisia za kwanini wameachana na mchezaji huyo ambaye ni miongoni mwa wanaofanya vizuri kwa sasa na ndipo Azam ilipotangaza sababu zake za kwanini hayo yametokea.
Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria amefafanua kuwa walimpa mapema Mudathir ofa ya mkataba mpya baada ya mkataba wake wa awali kumalizika Juni 30 mwaka huu lakini hakusaini mkataba huo mpaka mwezi Julai unamalizika na ndipo nao walipoamua kuchukua maamuzi.
“Baada ya kutamatika kwa mkataba wake Juni 30, akawekewa mezani mkataba mpya, hakuusaini, klabu ikaendelea kumsubiri mpaka Julai imeisha, hivyo hatua ya kwanza iliyofanyika ni kuitoa namba 27 aliyokuwa akiivaa na kupewa mchezaji mwingine, Malickou Ndoye.
“Tulifanya hivyo kwa sababu mchezaji tuliyekuwa tukimsubiri (Mudathir) hivyo timu ikaamua kuendelea na maisha mengine lakini kama nilivyosema kama ilivyo kwa wengine walioondoka tunawatakia maisha mema ya mpira huko waendako, na hapa Azam ni sehemu ya maisha yao muda wowote wakitaka kurudi hapa wanakaribishwa,” alisema Zakaria.
Mudathir ameondoka Azam baada ya kuitumikia tangu mwaka 2011 akiwa timu ya vijana kabla ya baadaye kupandishwa timu kubwa na msimu wa 2017/18 kupelekwa kwa mkopo Singida United alikoonesha kiwango kikubwa na kisha kurejea Azam msimu uliofuata.
Inaelezwa kuwa Mudathir tayari amemalizana na Singida Big Stars inayonolewa na kocha wa zamani wa Singida United, Hans van Der Pluijm ikiwa ni mipango ya kuiimarisha timu hiyo kuelekea msimu ujao.
Soka Mudathir akataa mkataba Azam
Mudathir akataa mkataba Azam
Read also