Munich, Ujerumani
Mshambuliaji mpya wa Barcelona, Robert Lewandowski hatimaye leo amekutana na kuagana rasmi na wachezaji na maofisa wa klabu yake ya zamani ya Bayern Munich na hivyo kuzika hali ya utata uliotokana na kuondoka kwake.
Lewandowski ambaye akiwa Bayern amejiwekea rekodi ya kuvutia ya kufunga mabao 344 katika mechi 375 na kutwaa mataji mbalimbali zikiwamo tuzo za mfungaji bora kwa miaka minane, amejiunga na Barca mwezi uliopita kwa ada inayofikia Euro milioni 45, uhamisho ambao aliulazimisha baada ya Bayern kuonekana kuwa wagumu na hivyo kuibua sintofahamu kati yake na klabu hiyo.
Tangu kuondoka Bayern, Lewandowski ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Poland, alijikuta katika hali ya kushutumiana na mabosi wake wa zamani huku mchezaji huyo akidai kwamba uhamisho wake ulijaa siasa nyingi kutoka Bayern ambao aliwashutumu kwa kujaribu kutafuta hoja ili wamuuze.
Bayern nao kwa upande wao walisema kwamba hali hiyo ilisababishwa na mchezaji huyo ambaye alikuwa akisisitiza kutaka kuhama licha ya kwamba alikuwa na mkataba ambao ulikuwa unafikia ukomo mwaka 2023.
“Kwa sasa kila kitu kiko vizuri, nimekutana na kila mtu na kuwashukuru, sitosahau nilichokipata hapa na uzoefu nilioupata, hilo ni jambo muhimu sana kwangu, wiki iliyopita kidogo kulikuwa na hali ya utata lakini kuna wakati haya ni mambo yanayotokea kwenye soka,” alisema Lewandowski katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Sky.
Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern, Hasan Salihamidzic alizungumza na Lewandowski kwa muda mfupi ambao mchezaji huyo alifika katika klabu hiyo na wameyaweka mambo sawa na hatimaye kuondoa utata uliojitokeza.
“Robert alikuja ofisini kwangu kuniaga na tumezungumza kwa dakika 15, nilimueleza kila kitu na tumeyaweka mambo sawa, Robert amefanya mambo makubwa hapa Bayern na hilo litabaki kuwa hivyo, naye pia anajua kwamba kwa nini anatakiwa kuishukuru Bayern,” alisema Salihamidzic.
Kimataifa Lewandowski, Bayern wazika tofauti
Lewandowski, Bayern wazika tofauti
Read also