London, England
Timu ya Taifa ya wanawake ya England, Lionesses, jana usiku ilitwaa Kombe la Ulaya (Euro 2022) baada ya kuilaza Ujerumani mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Wembley na kushuhudiwa na mashabiki wapatao 87,000.
Hilo linakuwa taji la kwanza kubwa kwa timu za soka za England tangu timu ya wanaume ibebe Kombe la Dunia mwaka 1966.
Wenyeji England ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 62 mfungaji akiwa ni Ella Toone bao lililochangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi binafsi za mchezaji huyo lakini Ujerumani walisawazisha dakika ya 79 kwa bao lililofungwa na Lina Magull na kuzifanya timu hizo zimalize dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.
Hatimaye England walizitumia vyema dakika 30 za nyongeza walipoandika bao katika dakika ya 110 mfungaji akiwa ni Chloe Kelly ambaye kama Toone wote walianzia kwenye benchi kabla ya kupewa nafasi ambazo walizitumia vizuri kuiwezesha England kubeba taji.
Ujerumani hata hivyo ilipata pigo baada ya mchezaji wake nyota ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo, Alex Popp kuumia wakati akijiandaa na mechi hiyo hali ambayo iliibua huzuni kwa mashabiki wa Ujerumani ambao walimtegemea mchezaji huyo kuiwakilisha vyema Ujerumani katika mechi hiyo.
Popp anayeichezea timu ya wanawake ya Bayern Munich pia alikuwa ndiye kinara wa mabao Ujeumani, tayari alikuwa na mabao sita katika mechi tano lakini kibaya zaidi ni kwamba hiyo inakuwa mara yake ya pili kuingia katika majanga ya aina hiyo baada ya kukosa michuano hiyo misimu miwili iliyopita kutokana na kuwa majeruhi.
Wachambuzi wengi wanaamini Ujerumani ilikwama sababu mojawapo ikiwa ni kukosa mtu mwenye nguvu na uwezo wa kuwaongoza wachezaji wenzake uwanjani kama aliokuwa nao Popp.
Kimataifa Wanawake England vinara Euro 2022
Wanawake England vinara Euro 2022
Read also