Manchester, England
Manchester United Jumapili usiku imetoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Rayo Vallecano, mechi ambayo Cristiano Ronaldo alicheza ingawa alitoka uwanjani kabla ya mpira kumalizika na hivyo kuendelea kuacha maswali kuhusu hatma yake katika klabu hiyo.
Juzi Ronaldo aliwapoza mashabiki wa Man United alipotuma ujumbe kupitia akaunti yake ya Instagram akiahidi angecheza mechi hiyo ya jana, kauli iliyotafsiriwa kuwa ameamua kubaki katika timu hiyo licha ya kutojiunga na wachezaji wenzake kwenye ziara ya kujiandaa na msimu wa 2022/23 katika nchi za Australia na Thailand kwa kilichoelezwa kuwa ni matatizo binafsi.
Ronaldo alicheza mechi hiyo kwa dakika 45 hakuweza kuisaidia timu yake kutoka uwanjani na ushindi ambapo kabla ya mechi kuanza aliwasalimia mashabiki wa Man United ambao nao walimuunga mkono kuonyesha kwamba hawakuwa na tatizo naye licha ya mchezaji huyo kuwa katika mjadala kwa siku za karibuni hasa baada ya kusisitiza kwamba anataka kuachana na timu hiyo
Katika mechi ya jana iliyopigwa kwenye Uwanja wa Old Traffod, United walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na kinda wa Ivory Coast, Amad Diallo dakika chache baada ya kuanza kipindi cha pili akimalizia kazi iliyofanywa na Alex Teles ambaye shuti lake liliokolewa kabla ya mfungaji kuuwahi mpira na kuujaza wavuni. Amad aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Ronaldo.
Bao hilo la United hata hivyo lilidumu kwa dakika tisa tu kabla Alvaro Garcia hajaisawazishia Vallecano na kuzifanya timu hizo zimalize mchezo zikiwa sare.
Wakati mechi ikiendelea Ronaldo alionekana akitoka uwanjani na hivyo kuibua maswali kwa mashabiki ingawa maofisa wa Man United hawakuwa tayari kusema kama mchezaji huyo aliruhusiwa kutoka mapema na kocha Erik ten Hag au aliamua tu kujiondokea.
Pia haijaweza kueleweka kwa kiwango alichokionyesha kwenye mechi hiyo kama mchezaji huyo atapata nafasi ya kucheza Agosti 7 wakati Man United itakapoanza mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England dhidi ya Brighton.
Kwa upande mwingine kocha Ten Hag ameeleza kufurahishwa na timu hiyo akisema kwamba kwa ujumla maandalizi yao yamekuwa mazuri ingawa pia bado wana nafasi ya kuweka mambo yao sawa na kuwa bora zaidi na ni lazima wafanye hivyo.
Kimataifa Ronaldo atoka uwanjani mechi ikiendelea
Ronaldo atoka uwanjani mechi ikiendelea
Read also