Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo baada ya kuwaeleza kuwa haondoki kokote licha ya kutakiwa na timu kadhaa ikiwemo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Mayele ambaye ndiye mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara akipachika mabao 16 amekuwa akitajwa kuwaniwa na vigogo kadhaa Afrika na kuibua hofu ya pengine mshambuliaji huyo raia wa DR Congo anaweza asiwepo Jangwani msimu ujao.
Mayele hata hivyo ameeleza kuwa licha ya kuwa na ofa nyingi lakini ameamua kubaki Yanga, jana akiwa ameanza rasmi maandalizi ya msimu ujao akiwa na timu hiyo iliyoweka kambi Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Ilikuwa ni kweli, timu zilikuwa nyingi zinanihitaji, iliyokuwa karibu kunichukua ni Kaizer Chiefs, Al Hilal ya Sudan na Raja Casablanca (Morocco) lakini mimi bado mchezaji wa Yanga nilisaini mkataba wa miaka miwili nimemaliza wa kwanza nimebaki na mwaka mmoja sasa.
“Namshukuru Mungu nimerejea tena kujiandaa na msimu mpya, tunahitaji kujiandaa vizuri kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao,” alisema Mayele aliyetua Yanga akitokea AS Vita.
Pia, Mayele amewaeleza mashabiki wa Yanga kuwa anafahamu kiu yao ya kutaka kumuona akifanya vizuri tena msimu ujao, hivyo yeye na wachezaji wenzake watajitahidi ili wawape zaidi ya kile wanachokihitaji mashabiki hao kwa kuzingatia mazoezi na maelekezo ya makocha.
Soka Mayele awashusha presha mashabiki
Mayele awashusha presha mashabiki
Read also