Na mwandishi wetu
Simba kesho inatarajia kucheza mchezo wake wa tatu wa kirafiki dhidi ya Haras El Hodoud katika kuendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23 wakiwa kambini kwao katika mji wa Ismailia nchini Misri.
Timu hiyo inacheza mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mechi yake ya kirafiki iliyocheza juzi na kuifumua Al-Akhdood mabao 6-0 huku mabao hayo yote yakifungwa na Pape Sakho aliyefunga mawili wakati mengine yalifungwa na Jonas Mkude, Meddie Kagere na Erasto Nyoni wakifunga moja kila mmoja.
Timu hiyo inayotarajiwa kurejea nchini Agosti 5, mwaka huu inaendelea kuimarika kama ilivyoelezwa na kocha mpya wa timu hiyo, Zoran Maki kutokana na programu walizonazo kambini hapo.
Katika mchezo wa kwanza wa kirafiki, Simba ilicheza dhidi ya Ismailia na kuambulia sare ya bao 1-1. Mechi hizo za kujipima nguvu, zimetajwa kama sehemu ya kukisuka na kuiunganisha vizuri timu hiyo ambayo inajipanga kurejea kwenye makali yake baada ya kupoteza makombe yote msimu uliopita.
“Kikosi changu kina mabadiliko mengi, kina wachezaji wengi wapya hivyo ili nijue ubora wao lazima niwaangalie kwenye mechi pia, wakicheza uwanja wa mazoezi pekee haitoshi kuwa kipimo cha ubora wa mchezaji,” alisema Maki.
Simba inatarajia kucheza mechi hiyo jijini Cairo dhidi ya Haras iliyopanda kushiriki Ligi Kuu Misri msimu ujao, ikionekana ni kipimo sahihi kwa Mnyama kulingana na ubora mkubwa waliouonyesha Haras msimu uliopita wakiwa Ligi Daraja la Pili Misri.
Soka Simba kuikabili El Hodoud
Simba kuikabili El Hodoud
Read also