Na mwandishi wetu
Kama sare tatu mfululizo ziliibua presha Yanga, basi ushindi wa mabao
2-0 ambao Simba imeupata jioni ya leo dhidi ya Kagera Sugar ni wazi
umezidisha presha Yanga.
Yanga inayoongoza Ligi Kuu ya NBC, imekuwa na matokeo ya sare tasa
tatu mfululizo, kwanza dhidi ya mahasimu wao Simba, Ruvu Shooting na
Prisons. Sare na Prisons ndiyo iliyoanza kuwafanya mashabiki wanazi wa
timu hiyo kuanza kujenga hisia kuwa mbio zao za kulinasa taji msimu
hii zimeanza kutikiswa.
Wako walioanza kutoa lawama kwa baadhi ya wachezaji baada ya sare hiyo
lakini kwa matokeo ya leo ya Simba ni dhahiri kwamba presha kwa
mashabiki Yanga itazidi kuongezeka huku wakijiuliza kulikoni na baadhi
kuanza kujenga hisia kwamba Simba wanaweza kuwashangaza wakati ligi
ikielekea ukingoni.
Jambo zuri ni kwamba Yanga bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 57
ikifuatiwa na Simba yenye pointi 49 na zote zimecheza mechi 23, hata
hivyo ukweli kwamba pengo la pointi limekuwa likipungua na sasa
zimebaki pointi nane.
Hiyo maana yake ni kwamba katika mechi saba zilizobaki katika ligi
hiyo, Yanga haipaswi kufanya kosa, kwani matokeo yoyote mabaya
yatakuwa au yanachelewesha timu hiyo kutangazwa bingwa au kuitoa
kabisa katika mbio hizo na kuipa Simba nafasi ya kutwaa taji la tano
mfululizo.
Katika mechi ya leo, Simba ilinufaika kwa mabao ya Dennis Kibu na John
Bocco, wakati mabao hayo yakizidisha presha Yanga, kwa mashabiki wa
Simba yameanza kuibua matumaini mapya ya timu yao kulinasa taji la
ligi hiyo kwa mara ya tano mfululizo.
Matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo kwanza yalitokana na matokeo ya
sare tatu za Yanga hasa ile ya Prisons na hapo hapo katikati ya sare
hizo wakawa na furaha ya ushindi wa mabao 4-1 ambao timu yao iliupata
dhidi ya Ruvu na leo ushindi mwingine wa mabao 2-0. Kwa sasa mashabiki
hao wanasubiri kwa hamu kujua nini kitatokea katika mechi zijazo za
Yanga.
Soka Simba yazidisha presha Yanga
Simba yazidisha presha Yanga
Read also