
Na Abdul Mohammed
Juni 17, 2008 kijana wa miaka 37 anatangazwa rasmi mbele ya jopo la waandishi wa habari kuwa ndiye kocha mpya wa klabu ya Barcelona akirithi mikoba ya Frank Rijkaard.
Kijana huyo ni Pep Guardiola, wakati anakabidhiwa majukumu hayo hakuwa na uzoefu wowote kutosha kuaminiwa kuinoa Barcelona au Barca, klabu maarufu, kubwa na yenye hadhi ya juu.
Tukio la kumkabidhi Pep klabu hiyo, mwandishi Guillem Balague alilifananisha na kucheza kamari, kwamba Barca walicheza kamari na hivyo uwezekano wa kocha huyo kukwama ulikuwa mkubwa tu na lisingekuwa jambo la ajabu hasa unapoangalia uzoefu aliokuwa nao wakati huo.
Uzoefu pekee katika kazi ya ukocha aliokuwa nao Pep wakati huo ni kwenye timu za vijana za Barca na timu ya wachezaji wa akiba, kazi aliyoifanya kuanzia mwaka 2007.

Hadi wakati anatangazwa mara ya kwanza kuwa mrithi wa Rijkaard, makubaliano yalikuwa ya mkataba wa miaka miwili licha ya wakala wake, Josep Maria Orobigt kutaka uongezwe mwaka wa tatu na malipo ya bonasi iwapo atashinda moja ya mataji matatu muhimu lakini makubaliano hayakufikiwa.
Balague na wengine walikuwa na kila sababu ya kuuona uteuzi wa Pep kuwa sawa na kucheza kamari kwani katika historia ya Barca haikuwahi kutokea kwa mtoto muokota mipira wa Nou Camp, aliyecheza ngazi zote za timu ya vijana hadi timu ya kubwa na kuwa nahodha halafu baadaye akawa kocha.
Ukweli kwamba uteuzi wa Pep katika nafasi hiyo ulihusisha watu wanaoitwa football brains (wenye akili za soka-tafsiri yangu) wa Barca haukutosha kuwatoa wasiwasi manazi wa klabu hiyo maarufu ‘Cules’ kuamini kwamba Pep ni chaguo sahihi.
Ni kutokana na hali hiyo, Rais wa klabu, Joan Laporta akawa na kazi ya kuwaambia waandishi wa habari ni kwa nini Pep na si makocha wengine wenye hadhi waliokuwa wakitajwatajwa kuwa warithi sahihi wa Rijkaard akiwamo Jose Mourinho.
Laporta aliwaambia waandishi wa habari, “tumemchagua Pep kutokana na uelewa wake wa soka, anaijua vyema klabu hii na anapenda soka la kushambulia, ni mtu wa soka mwenye akili ya soka lakini pia ni mwenye uelewa na wakati wote yuko makini, wakati wote anafikiria soka.’’
Kazi ya kwanza ngumu kwa Pep ambayo ilishangaza wengi ni pale alipotangaza kwamba Ronaldinho, Deco na Samuel Eto’o hawakuwa katika mipango yake katika klabu hiyo ingawa kwa Eto’o baadaye alibadili mawazo.
Ronaldinho pamoja na kuwa fundi wa mpira lakini Pep alimkataa mapema na kumuuza AC Milan wakati Deco aliuzwa Chelsea. Mastaa wengine wenye majina makubwa ambao Pep aliwatoa katika mipango yake ya Barcelona ni Giovani dos Santos, EdmÃlson na Gianluca Zambrotta.
Kilichofuata baada ya hapo ulimwengu wa soka unakifahamu, leo hii ukiizungumzia miaka minne ya Pep na Barca, unamzungumzia kocha aliyeweka rekodi ya kipekee, mataji matatu mfululizo ya La Liga, mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mawili ya Uefa Super Cup na mawili ya Kombe la Dunia la klabu. Pia utakuwa unamzungumzia kocha aliyefanikiwa kuufanya mpira kuwa burudani.
Baada ya kutoka tu Barca Pep akawa kwenye mapumziko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuanza tena kibarua Bayern Munich na sasa Man City.
Miaka 13 sasa imepita tangu Pep apewe nafasi hiyo na kuweka rekodi ya kuvutia, kwa mara nyingine Barca wameamua kumpa kazi hiyo Xavi Hernandez ambaye anakabidhiwa timu hiyo akiwa na miaka 41 tofauti na Pep aliyekabidhiwa akiwa na miaka 37.
Ukiachana na uzoefu wa kwenye timu za vijana ambao ndio aliokuwa nao Pep wakati akikabidhiwa kibarua cha kuinoa Barca, tofauti yake na Xavi mbali na umri ni kwamba Xavi yeye ameanzia katika klabu ya Al Sadd ya Qatar ambayo alianza kuinoa Mei, 2019.
Al Sadd ni klabu ya Ligi Kuu ambayo aliiwezesha kufikia hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Asia na kutwaa taji la ligi mara moja na mataji mengine mawili. Mafanikio hayo kimsingi au katika hali ya kawaida hayatoshi kuwa sababu ya Xavi kukabidhiwa jukumu la kuinoa Barca.
Kwa kuzingatia uzoefu na mafanikio ya Xavi na hadhi ya Barca inaweza kuonekana kama Barca imecheza kamari nyingine kwa Xavi kama ilivyofanya kwa Pep lakini ni wazi kwamba yapo matumaini tena makubwa tu kwamba kamari ya Xavi italipa kama ilivyolipa kwa Pep.
Ukiachana na Al Sadd, Xavi kama ilivyo kwa Pep naye ni zao la La Masia, shule ya soka kwa vijana iliyozalisha mastaa wengi walioibeba vyema klabu hiyo wakiwamo kina Cesc Fabregas, Lionell Messi na wengineo.
Kwa maana nyingine kama alivyo Pep, Xavi naye analijua vyema aina ya soka la Barca au anaujua vyema utamaduni wa klabu hiyo, uzoefu ambao hapana shaka huenda ukamsaidia kama ulivyomsaidia Pep kuifikisha klabu hiyo mbali.
Enzi zao Xavi na Pep wakicheza soka la ushindani wote walikuwa nafasi za kiungo ingawa Pep alikuwa kiungo mkabaji zaidi na Xavi kiungo mchezeshaji, lakini wote walikuwa zinazofanana wakiwa uwanjani, sifa ya kuusoma mchezo na kuwa wabunifu.
Katika hili, Pep wakati wote alisifika si tu kwa kuusoma mchezo bali kutabiri kinachofuata hasa pale anapopewa pasi, kabla mpira haujafika miguuni mwake alikuwa akitabiri au kufikiria nini kitafuata au nini atakifanya, kama ni kumpasia mchezaji mwingine vipi usalama wa mchezaji huyo dhidi ya wachezaji wa timu pinzania na kama ni kumrudishia aliyempa mpira nini kitafuata baada ya hapo, alijua au kutabiri kitakachofuata au nini afanye ili timu iende mbele.
Hiyo pia ni tabia ya Xavi akiwa kiungo zama zake Barca na hata kwenye timu ya Taifa ya Hispania, huo ndio uliokuwa utaratibu wake au staili yake ya uchezaji, ni aina ya wachezaji ambao unaweza kuwaita wana akili ya soka au football brain (tafsiri yangu) lakini pia ni wabunifu.
Pia walikuwa ni aina ya wachezaji mahiri katika kutoa pasi za uhakika, kwa Pep hili lilimbeba sana kwani, hakuwa mwenye mwili uliojazia bali akiwa kiungo mkabaji au hata alipokuwa kiungo wa kati, alisifika kwa kuvuruga mipango ya timu pinzani kwa namna alivyokuwa akijua nini kinafuata na akiwa na mpira basi kinachofuata ni pasi ya uhakika.
Wote si waumini wa soka la kutumia mabavu bali ni taratibu, mbinu nyingi, kufungua uwanja na kuuchezea mpira katika kusaka ushindi.
Pep alipokabidhiwa Barca kitendo cha kumkataa Ronaldinho kiliwashangaza baadhi ya watu lakini hapo hapo kulikuwa na habari kwamba mchezaji huyo alishakuwa ‘kigogo’ hakuwa tena wa kupangiwa fanya hivi au vile. Hili ni jambo ambalo Pep alilikataa kwani dhamira yake ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha yeye anakuwa juu kwenye timu, akaweka taratibu na kutaka ziheshimiwe.
Kwa Xavi naye dalili za hilo zimeshaanza kuonekana, dalili za kujenga himaya yake na kutaka kuhehimiwa na kila mchezaji na kuwa mwenye sauti ya mwisho, ameshaweka taratibu zake anazotaka ziheshimiwe, tayari ameanza kumnyooshea kidole, Dembele kwa kumuadhibu kwa kuchelewa mazoezini.
Inadaiwa kosa la Dembele kuchelewa halikuwa kubwa kwani taarifa zinadai alichelewa dakika tatu na taarifa nyingine zinadai hakuchelewa zaidi ya dakika tano japo huko nyuma ilikuwa jambo la kawaida kwake lakini katika kujenga himaya yake Xavi ameamuru mchezaji huyo akatwe mshahara.
Mchezaji mwingine aliyekumbana na taratibu mpya za Xavi ni beki mkongwe Gerard Pique naye amepigwa marufuku kushiriki katika vipindi maarufu vya televisheni.
Mwanzo wa Xavi umekuwa mgumu, ametolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati kwa Pep alianza vizuri hadi kutamba, hapo hapo kuna ukweli kwamba Xavi ameanzia katikati ya msimu wakati Pep alianzia mwanzo wa msimu. Pengine kwa kutambua hilo ndiyo maana kitendo cha Barca kutolewa katika Ligi ya Mabingwa, Xavi amekiita kuwa ni mwanzo wa zama mpya.
Kwa hali hiyo si vibaya kujenga imani kwamba huenda miaka ijayo Barca ya Pep ikarudi safari hii dereva akiwa ni Xavi.